John Heche alikamatwa na polisi mara tu baada ya kuingia katika geti kuu la Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam Jumatano saa tatu asubuhi. Alikuwa amefika mahakamani hapo kufuatilia kesi mbili — ile ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini na kesi nyingine inayohusu matumizi ya rasilimali za chama ambayo pia ilikuwa inasikilizwa Jumatano.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya tukio hilo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika alisema hadi sasa hawajapewa taarifa rasmi kuhusu sababu za kukamatwa kwa Heche lakini akagusia uwezekano wa tukio hilo kuhusiana na mgogoro wa Heche na Idara ya Uhamiaji.

Wiki iliyopita, Heche alizuiliwa na maofisa wa Idara ya Uhamiaji katika eneo la Isibania, mpakani mwa Tanzania na Kenya mkoani Mara, alipokuwa akielekea kwenye mazishi ya kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Hayati Raila Odinga.

Tanzania Dar es Salaam 2025 | Kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tundu Lissu
Mwenyekiti wa Chama cha Upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu akiwa mahakamaniPicha: Ericky Boniphace/DW

Baada ya tukio hilo, Idara ya Uhamiaji ilitoa taarifa ikidai kwamba kiongozi huyo alivuka mpaka na kuingia Kenya bila kufuata taratibu za kisheria za uhamiaji.

Juhudi za kuwapata maafisa polisi hazikufanikiwa

Juhudi za kuwapata maofisa wa polisi ili kutoa ufafanuzi kuhusu sababu za kukamatwa kwa Heche hazikufanikiwa hadi tunapokwenda mitamboni.

Wakati huo huo, katika Mahakama Kuu, Jaji Dunstan Ndunguru ametoa uamuzi mdogo katika kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu baada ya upande wa utetezi kuwasilisha pingamizi dhidi ya shahidi wa upande wa Jamhuri aliyejitambulisha kama mtaalamu wa picha.

Lissu aliieleza Mahakama kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kisheria kuwasilisha kielelezo hicho, kwa kuwa yeye ni mtaalamu wa picha za mnato, na si mtaalamu wa picha jongefu (video), kama kesi hiyo inavyohitaji.

Jaji Ndunguru alikubaliana na hoja za Lissu, akisema shahidi huyo hana mamlaka ya kisheria kuwasilisha ushahidi huo mahakamani. Kesi ya msingi ya uhaini dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu inaendelea kusikilizwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *