Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikielekea katika uchaguzi mkuu ujao, wananchi wameainisha mambo 11 wanayotaka yawe miongoni mwa vipaumbele vya Rais ajaye ndani ya siku 100 za kwanza baada ya kuapishwa.

Mambo hayo yamebainishwa kupitia utafiti uliofanywa kwa siku nne kuanzia Oktoba 15, 2025 na Asasi ya Vijana na Wanawake (Tafeyeco) katika wilaya zote za mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mambo hayo yanahusu zaidi masuala ya huduma za kijamii, haki za kiuchumi, uwajibikaji wa viongozi na mageuzi katika sekta muhimu kama elimu, afya na miundombinu.

Utafiti huo ulilenga kupata maoni ya wananchi kuhusu matarajio yao kwa Rais ajaye katika kipindi cha awali cha uongozi wake.

Katika utafiti huo, wananchi 1,200 walishiriki kwa kutoa maoni yao, ambapo wengi wao waliorodhesha mambo 11 wanayotamani yawekwe kipaumbele na Rais atakayechaguliwa, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja hadi miezi mitatu baada ya kuapishwa.

Miongoni mwa mambo hayo, ni Rais ajaye awaingize wapinzani kwenye Serikali yake kwa kuwateua katika nafasi mbalimbali sanjari na kuunda kamati ya maridhiano itakayowaleta Watanzania pamoja.

Mbali na wananchi, wadau wa masuala ya kisiasa nchini wameonyesha mitazamo tofauti kwa Rais atakayechaguliwa, baadhi yao wakiungana na wananchi kutoa maoni ya vitu gani wanatamani avifanye mara tu baada ya kuapishwa.

Usemavyo utafiti

Tafeyeco kwenye utafiti wake uliofanyika kwenye wilaya zote za mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, imebainisha wananchi wanaamini mambo hayo 11 yatatekelezwa yatasaidia kuimarisha umoja kwa Watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Oktoba 21, 2025 wakati akiwasilisha ripoti ya utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji Tafeyeco, Elvice Makumbo amesema jambo la kwanza lililotajwa kwa wingi na wananchi hao ni Rais ajaye awaingize wapinzani kwenye Serikali yake kwa kuwateua katika nafasi mbalimbali na si kuteua viongozi wa chama chake pekee.

Jambo la pili ni kuundwa kwa kamati ya maridhiano itakayowaleta Watanzania pamoja, kamati ambayo wametaka iwahusishe wazee wenye ushawishi nchini, viongozi wa dini, wanasiasa, wanaharakati na watu kutoka asasi za kiraia.

Amesema katika maoni yaliyohusisha watu 1,200 wenye umri wa kupiga kura, wanawake wakiwa 768 na wanaume 432 na kati yao vijana wa miaka 18-25 wakiwa ni 578, kwa nyakati tofauti wameeleza nini ambacho wanatamani Rais ajaye akifanye na mambo hayo 11 yamejirudia mara nyingi.

Mambo mengine waliyoyataka ni Rais atakapoapishwa atoe msamaha kwa Watanzania waliopo magerezani kwa sababu za kisiasa.

akifafanua hilo, Makumbo amesema hayo yalikuwa maoni ya ujumla ya wananchi, hivyo yawezekana ni wengi wapo magerezani kwa sababu za kisiasa, hivyo matamanio ya wananchi ni Rais ajaye kuwasamehe wote ili kuleta mshikamano wa kitaifa.

Jambo la nne walilotaka wananchi ni kuundwa kwa sheria itakayozuia watu kuleta uasi na uchochezi sanjari na matumizi sahihi ya mitandao.

Jambo la tano ni kujengwa miundombinu, ikiwamo barabara kubwa ya Dar es Salaam hadi Chalinze na kujenga madaraja ya juu katika makutano yote ya barabara za Dar es Salaam.

Jambo jingine ambalo limejirudia mara kwa mara katika maoni ya utafiti wa Tafeyeco ni mchakato wa Katiba mpya na kusimamia kwa uhakika upatikanaji wa maji na umeme katika mikoa hiyo.

“Jambo la nane ni Rais ajaye kupunguza gharama za bando kwenye mitandao ya simu.

“Ili limeombwa sana na vijana ambao katika maswali tuliyowauliza wamesema hivi sasa dunia ipo mtandaoni, lakini gharama ya mabando ni kubwa ambayo wengi wanashindwa kuimudu,” amesema.

Mengine ni vyombo vya ulinzi na usalama kutotoa tenda ya vifaa vyao kwa watu binafsi, kukomesha matukio ya watu kutekwa, kupotea na kuuawa na kuongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

“Wengi wamesema isiangaliwe anayestahili mkopo ametoka shule gani kidato cha sita au chuo gani cha diploma ametoka, fursa hiyo itolewe bila kujali shule wala chuo gani ametoka,” amesema.

Mbali na mambo hayo 11, Makumbo amesema katika utafiti huo waliwauliza pia endapo wanahudhuria kwenye mikutano ya kampeni inayoendelea kote nchini ambapo asilimia 75 walikiri kuhudhuria na waliobaki hawahudhurii, vilevile asilimia 97 wameeleza kufuatilia mikutano ya kampeni kwa njia mbalimbali ikiwamo mitandao ya kijamii na asilimia tatu hawafuatilii.

Mmoja wa vijana Leken Toima aliyeshiriki katika maoni hayo amesema alichokibaini ni kile kinachozungumzwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uchaguzi ni tofauti na uhalisia.

“Wakati tukipokea maoni, wengi tuliozungumza nao ikiwamo vijana wanahamasika kupiga kura, japo wameomba baadhi ya mambo yafanyike mara tu baada ya uchaguzi,” amesema.

Wasomi, wachambuzi waongezea

Akizungumzia utafiti huo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye yeye amegusia masuala ya kiuchumi, akisisitiza kwamba Rais atakayechaguliwa ausimamie kikamilifu ili ukuaji wake unaotegemewa ufikiwe vema.

“Natamani Rais ajaye asimamie hilo ipasavyo, ili ukuaji wa uchumi tunaoutegemea na mtazamo wa Dira ya Maendeleo viweze kufikiwa vema,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Dk Sabatho Nyamsenda yeye ametaja mambo manne anayotamani Rais ajaye ayafanye akibainisha kwamba asome alama za ukutani, ni aina gani ya taifa ambalo anaingia kuliongoza, akieleza kwa sasa lina migawanyiko ya kisiasa, kidini, kikanda na mingineyo.

“Kitu cha kwanza ni kuchukua hatua ili kujenga umoja wa kitaifa, ambao hautumii mabavu, kwa  kuwaleta watu pamoja na kuwa na wazo la pamoja ambalo kila mtu anavyoliona hilo anaona litaleta matumaini,” amesema.

Amesema jingine ni kujenga imani na taasisi za Serikali na vyombo vingine vya dola, hali ambayo huko mtaani watu wengi ni kama wamepoteza imani, hivyo Rais ajaye arudishe imani hiyo kwa wananchi.

“Vilevile matumizi makubwa ya mabavu kwenye vyombo vya dola nayo yanapaswa kuangaliwa na jambo la nne ni kuondoa pengo lililopo kati ya walionacho na wasionacho.

“Watu wanaona kuna watu wana mapesa (fedha) ya ghafla wanatamba kwenye mitandao ya kijamii na  haieleweki yanatoka wapi? Kuna pengo kubwa la walionacho na wasionacho, kutokuwepo kwa ajira, wengi sana hawana ajira, kwa matiki hiyo anapaswa kuongoza mageuzi ya kiuchumi,” amesema Dk Nyamsenda.

Kwa upande wake, Profesa Mohammed Bakari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema hali ya kisiasa iliyopo si nzuri, jamii ikionekana kuendelea kugawika kwa itikadi za vyama, akiamini katika hali ya kisiasa nchi imerudi nyuma.

“Tumerudi nyuma kuliko huko nyuma, natamani Rais atakayechaguliwa aweke utaratibu wa kuhuisha mchakato wa Katiba mpya ili tusije kuingia kwenye uchaguzi mwingine katika hali kama hii iliyopo,” amesema.

Amesema hoja za katiba iwe kipaumbele kwa Rais atakayechaguliwa ili baada ya uchaguzi huu, ule utakaofuata mwaka 2030 kusiwe na malalamiko kama yanayojitokeza sasa na yale yaliyotokea 2020,” amesema.

Kwa upande wake, Dk Richard Mbunda wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa upande wake anasema hali iliyopo, watu wengi wanadhani kuna chama kimejitwalia fursa zozote na hatamu ya nchi.

“Hii inamaanisha kwamba kimeshikilia kila pembe na ndicho kinachopigiwa kelele, pia tunaona kauli nyingi za ajabu zinatolewa, nafikiri baada ya uchaguzi kuwe na namna ya kauli ambazo zitaliponya taifa,  si za kutishana,” amesema.

Naye mchambuzi wa siasa za kimataifa, Said Msonda amebainisha kwamba Rais ajaye ahakikishe anashughulikia hoja ambazo zinaibuliwa na wananchi mara kwa mara.

“Hoja ni nyingi, Rais anatakiwa ahudumie watu kwenye masuala ya miundombinu, maboresho afya, kilimo, na kada nyingine, hata hivyo ahakikishe anatimiza mahitaji ya makundi jamii, mengi yana mahitaji, lakini kwenye eneo la wanasiasa lina changamoto za kipekee.

“Japo wanasiasa wengi huwa wanatanguliza masilahi binafsi, Rais ajaye awasikilize wana hoja gani na azifanyie kazi, ipo haja ya kupata maridhiano na muafaka atakapoingia madarakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *