TIMU ya TRA United imeshindwa kutamba nyumbani kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, baada ya leo Oktoba 22, 2025 kulazimishwa suluhu (0-0) dhidi ya Mashujaa, ikiwa ni sare ya tatu mfululizo kwa kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute kwa dakika zote 90, licha ya wachezaji wa timu zote mbili kushambuliana kwa zamu, lakini umakini ulikosekana wa kutumia vyema nafasi za kufunga, hivyo kusababisha pambano hilo kuisha kwa suluhu.

Suluhu ya leo, inaifanya TRA kutoka sare ya tatu mfululizo katika Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya timu hiyo kufungana mabao 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji nyumbani, Septemba 20, 2025, kisha 0-0 mbele ya Pamba Jiji ugenini, Septemba 28, 2025.

Kwa upande wa Mashujaa ambayo hii ni mechi ya tano msimu huu, inakuwa sare ya pili baada ya kufungana bao 1-1 dhidi ya maafande wenzao wa kikosi cha JKT Tanzania, Septemba 18, 2025, kisha kushinda 1-0, mbele ya Mtibwa Sugar, Septemba 21, 2025.

Baada ya hapo, kikosi hicho kikachapwa mechi mbili mfululizo, kikianza na bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars, Septemba 30, 2025, kisha pambano la mwisho kabla ya hili, ikachapwa na Pamba Jiji mabao 2-1, Oktoba 17, 2025.

Suluhu ya leo, inaifanya TRA ambayo zamani ilikuwa Tabora United kulinda ubabe wake mbele ya Mashujaa, kwani kikosi hicho tangu kipande Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, hakijawahi kupoteza kikiwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora dhidi ya wapinzani hao.

Msimu wa 2023-2024, TRA ilishinda bao 1-0 kupitia aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo raia wa Ghana, Eric Okutu, katika mechi iliyopigwa Mei 12, 2024, ikiwa ni ya marudiano, baada ya pambano la kwanza ugenini kuisha kwa sare ya bao 1-1, Desemba 5, 2023.

Msimu wa 2024-2025, TRA ilishinda bao 1-0, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, lililofungwa kwa penalti na Morice Chukwu dakika ya 8, Novemba 4, 2024, kisha Mashujaa ikalipiza kisasi mzunguko wa pili kwa kushinda mabao 3-0, Aprili 10, 2025.

Kwa matokeo ya leo, yanaifanya TRA kubakia nafasi ya 14 na pointi tatu, baada ya kucheza mechi tatu na kutoka sare zote, huku Mashujaa ikiwa nafasi ya sita na pointi tano, kufuatia kucheza mechi tano, ikishinda moja, sare mbili na kuchapwa mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *