Katika historia ya uchaguzi duniani kote, ushindani huwa ni jambo la kawaida, hasa katika nchi zenye mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, ushindani huo hauchochewi tu na wingi wa vyama, bali na ushawishi wa vyama vyenye nguvu zinazolingana. Hali hiyo haijajitokeza kwa kiwango kikubwa nchini Tanzania, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kutawala tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Ingawa Tanzania ina vyama vya siasa vilivyosajiliwa 19, chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kimejiondoa kwenye uchaguzi kwa madai ya kutokuwepo kwa mazingira ya haki, wakisisitiza kauli mbiu ya “Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi.” Kutokuwepo kwa CHADEMA kumetoa nafasi kwa  CCM kufanya kampeni bila upinzani mkubwa uliozoeleka.

Vyama vyakabiliwa na changamoto

Vyama vingine vinakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na chama tawala, huku ACT-Wazalendo ikikumbwa na mgogoro baada ya mgombea wake wa urais, Luhaga Mpina, kuenguliwa na Tume ya Uchaguzi kufuatia pingamizi kutoka kwa mwanachama wa chama hicho. Ingawa walikata rufaa mahakamani, ila bado hali kwa upande wao si ya kuridhisha.

Uchaguzi Tanzania 2025: Watanzania Wanataka Nini Kibadilike?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mchambuzi wa siasa Paternus Niyegira anasema hali ya kisiasa nchini Tanzania inaweza kugawanywa katika makundi matatu. Kundi la kwanza linajumuisha wafuasi wa CCM, ambao wana matumaini makubwa kuhusu mchakato wa uchaguzi na matokeo yanayotarajiwa.

Kundi la pili linajumuisha wafuasi wa vyama vya upinzani, wakiwemo wa CHADEMA na ACT-Wazalendo, ambao wanaamini kuwa mchakato wa uchaguzi hauna uwazi wala usawa. Kundi la tatu linatokana na mitandao ya kijamii, likitoa wito wa maandamano ya kitaifa Oktoba 29 hali inayoongeza mvutano katika siasa za Tanzania.

Serikali yajibu kwa kulaani maandamano

Serikali imejibu kwa kutoa matamko kadhaa ya kulaani maandamano hayo yanayopangwa, ikisisitiza umuhimu wa amani na utulivu. Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewahakikishia raia kuwa hali ya usalama ndani ya nchi na mipakani ni tulivu na imara.

Picha ya Logo ya Tume ya uchaguzi nchini Tanzania 2025
Nembo ya Uchaguzi wa Tanzania wa 2025. Picha na: INEC, TanzaniaPicha: INEC/Tanzania

Hata hivyo, Niyegira anasema bado kuna wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusu yatakayojiri siku ya uchaguzi, ingawa maafisa wa serikali wanaendelea kuwahakikishia wananchi kuwa mchakato utaendelea kwa amani na utulivu.

Dkt. Bravious Kahyoza ni mtaalam wa masuala ya uchumi anasema katika nchi nyingi zinazoendelea, uchumi huathiriwa na jinsi uchaguzi unavyosimamiwa  ambapo mvutano wa kisiasa unaweza kusababisha mshtuko wa kiuchumi. Anaeleza kuwa hali ya kisiasa na kiuchumi ya Tanzania kwa sasa ni tulivu, ikionyesha uwezekano wa uchaguzi wa amani na kuendelea kwa uthabiti wa kiuchumi.

“Uchumi huendeshwa kwa imani, na kwa sasa imani hiyo inaonekana kuwa imara. Ingawa tathmini kamili hufanyika baada ya uchaguzi, viashiria vya sasa vinaonyesha hali nzuri,” amesema Dkt. Kahyoza. Ukuaji wa uchumi uko juu ya asilimia 5, huku mfumuko wa beiukiwa katika kiwango cha kudhibitiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *