Mbeya. Zikiwa zimebakia siku saba Watanzania wapige kura katika Uchaguzi Mkuu wa Jumatano Oktoba 29, mgombea ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Ipyana Njiku ameanza kuzisaka kura mtaa kwa mtaa.
Miongoni mwa maeneo ambayo anayafikia kwa urahisi ni pamoja na vijiwe vya bodaboda, bajaji wakiwepo kina mama wajasiriamali wa mboga na matunda kwenye masoko.
Staili ya mgombea huyo imekuwa kivutio na kukusanya wananchi wakiwepo kina mama kusikiliza sera zake na nini atatekeleza endapo akipewa ridhaa ya kuwatumikia.
Awali, akizungumza na wananchi wa makundi mbalimbali, Njiku ametaja moja ya kipaumbele cha kwanza ni kutatua hadha ya maji katika Bonde la Uyole sambamba na ujenzi wa soko la kisasa ili kuondoa hadha kina mama kukaa juani.
Njiku amesema yeye ni mkazi Kata ya Nsalaga Bonde la Uyole, anatambua kero ya maji iliyopo kwa kipindi kirefu, endapo akipata ridhaa atahakikisha anaishawishi Serikali kufikisha huduma ya maji safi na salama kutoka chanzo cha Ziwa Nyasa Wilaya ya Kyela.
“Nimekuja kuomba kura zenu Oktoba 29, mwaka huu mkachague Chaumma, kwani natambua kuna tatizo kubwa la maji safi na salama na nyinyine nyingi, ndio sababu iliyo nisukuma kuja kwenu kuomba ridhaa ya nafasi hii niwe mwakilishi wenu bungeni mjini Dodoma,” amesema.

Mgombea ubunge Uyole kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma(Chaumma),Ipyana Njiku akizungumza na mmoja wa wajasiriamali Soko la Uyole wakati akiomba kura na kuhamasisha kujitokeza kushiriki uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025. Picha na Hawa Mathias
Njiku, amesema mbali na kuboresha huduma ya maji, lakini watazingatia vipaumbele vya wananchi lengo ni kuona wanafikishiwa huduma karibu zikiwepo sekta ya elimu na afya.
“Tunajua changamoto za wananchi nimekuja kwenu mtupe kura za kishindo za nafasi ya Rais, wabunge na madiwani kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025, ili tuweze kufanya yale tulio waeleleza kwenye mikutano ya kampeni lengo ni kuleta maendeleo kwa wana Uyole,”amesema.

Mkazi wa Uyole, David Aloyce amesema wao wako kuangalia sera na chama kitakacho leta maendeleo kikubwa ni kuibua changamoto za wananchi na kuzitatua hususani katika kusimamia sera zao.
“Wagombea mbalimbali wanakuja na sera zao za kuleta maendeleo wa Watanzania, lakini wanapaswa kutambua kura ni siri ya mpiga kura ambaye anajua nani atampigia,” amesema.