Kiasi kikubwa cha fedha kinachokusanywa kwa ajili ya ujenzi upya wa Syria kimewashangaza wengi. Baadhi wanatizama kama muujiza wa kipekee. Michango hiyo, ambayo imekuwa ikiendelea tangu katikati ya Agosti mwaka uliopita, huenda ndiyo kampeni ya kuchangisha fedha iliyofanikiwa zaidi duniani. Je, hii ni dalili ya matumaini mapya ya kuijenga upya Syria, au ni mbinu ya baadhi ya watu kujisafisha mbele ya umma?
Mnamo mwaka 2024, wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais nchini Marekani, mgombea wa chama cha Democratic, Kamala Harris, alifanikiwa kukusanya zaidi ya dola milioni 47 chini ya saa 24 pekee kutoka kwa wafadhili wake.
Lakini mnamo mwezi Septemba, katika muda sawa, wafadhili huko Idlib, kaskazini mwa Syria, walichangisha takriban dola milioni 208, kiwango kikubwa kisichotarajiwa kwa nchi iliyokumbwa na vita kwa zaidi ya muongo mmoja.
Tangu katikati ya msimu wa kiangazi, kumefanyika takriban kampeni10 katika miji na wilaya mbalimbali nchini humo zenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi upya wa Syria.
Kampeni tofauti katika miji na wilaya tofauti
Kiasi cha fedha kinachopatikana katika kila kampeni kimeripotiwa na vyombo vya habari vya ndani, ingawa takwimu hizo ni vigumu kuthibitishwa na mashirika huru. Kwa mujibu wa nyaraka ambazo DW imeziona, fedha zote zilizokusanywa zinakaribia dola milioni 500.
Kampeni hizo zimepokelewa kwa shangwe na matumaini makubwa. Kwa Wasyria wengi, ni ishara ya matumaini mapya kwamba nchi yao, iliyoharibiwa vibaya na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muda mrefu, inaweza kufufuliwa tena.
Fadel al-Akl, mwanachama wa kamati ya ukusanyaji fedha tawi la Idlib, amesema kampeni hizo zimejikita katika misingi ya umoja na ushirikiano wa kitaifa.
Soma zaidi kuhusu Syria baada ya al-Assad
Akizungumza na DW, alisema hatua ya kwanza ni kurejesha hali ya kawaida katika vijiji na miji ambako hakuna tena miundombinu, shule, vituo vya afya wala mifumo ya maji. Amesema kampeni hizo zimehusisha watu wa rika na tabaka zote kuanzia matajiri hadi masikini.
Je, wachangiaji wanatoa kwa moyo wa dhati au wanajitakasa?
Wachangiaji wengi wanatoa fedha ndogo kuanzia dola nne, huku mchangiaji mkubwa akiwa ni Ghassan Aboud, bilionea wa Kisyria anayeishi Umoja wa Falme za Kiarabu, ambaye alitoa dola milioni 55 peke yake. Awali, Aboud alionekana kuwa mpinzani wa serikali ya Bashar al-Assad, jambo lililoibua mjadala kuhusu motisha yake ya sasa.
Hata hivyo, si wote wanaoamini nia njema ya michango hiyo. Mwezi Oktoba, mtafiti wa taasisi ya Chatham House ya Uingereza, Haid Haid, aliandika kuhusu jinsi familia tajiri ya Hamsho, inayodaiwa kuwa na uhusiano wa kihalifu na utawala wa zamani wa Assad, ilivyotoa mamilioni ya dola kupitia kampeni mbili tofauti.
Mkaazi mmoja wa Idlib, ambaye hakutaka kutajwa jina, ameiambia DW kwamba baadhi ya wachangiaji wanatoa kwa moyo wa dhati, lakini wapo pia wanaotumia kampeni hizo kama njia ya kujisafisha dhidi ya makosa ya zamani.
Maswali bado yanaibuka kuhusu uwazi wa matumizi ya fedha hizo, nani anazisimamia, na iwapo zitaelekezwa kweli katika ujenzi wa nchi, au zitakuwa chombo cha kisiasa cha kujenga taswira mpya mbele ya umma wa Syria na dunia.