Fatemeh Mohajerani Msemaji wa serikali ya Iran amesema kuwa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoidhinisha makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 limekwisha muda wake na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelitaarifu Baraza la usalama kuhusu kumalizika muda huo.

Akizungumza katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari jana Jumanne, Mohajerani amesema kuwa Iran, Russia na China kwa pamoja zimetuma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zikitangaza kumalizika muda wa azimio nambari 2231. 

“Iran, Russia na China zinaona kuwa hakuna msingi wowote wa kuendelea na majadiliano kuhusu suala hilo na Baraza la Usalama halijachukua hatua yoyote kuhuisha maazimio yaliyositishwa huko nyuma,” amesema Msemaji wa serikali ya Iran. 

Bi Fatemeh Mohajerani aidha amesisitiza kuwa sehemu kubwa ya jamii ya kimataifa inapinga hatua na misimamo ya upande mmoja kuhusu masuala ya dunia. 

Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama muda wake ulimalizika tarehe 18 mwezi huu wa Oktoba na hiyo kufikisha miaka kumi tangu lilipowasilishwa. Mwezi Agosti mwaka huu, nchi tatu za Ulaya Uingereza, Ujerumani na Ufaransa maarufu kwa jina la Troika ya Ulaya zilirejesha utaratibu kwa jina la Snapback zikitaka kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran ambavyo viliondolewa kwa mujibu wa makubaliano ya mwaka 2015. 

Hata hivyo, Iran, Russia na China zinasisitiza kuwa kwa kuwa Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama limekwisha muda wake, jaribio lolote la kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa ni batili , na Iran haipasi tena kukabiliwa na hatua hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *