
AWALI, wakati wanamchukua, maafisa hao walimhisi Muddy alikuwa akijihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya. Walianza kumpekua hatua kwa hatua na kwa umakini mkubwa.
Waliipitisha mizigo yake katika sehemu maalumu ambayo ilikuwa na mbwa waliokuwa wamepewa mafunzo ya kubaini dawa za kulevya uwanjani hapo lakini hakubainika kama alikuwa amebeba kitu chochote cha hatari. Achana na dawa za kulevya.
Kitu walichomkuta nacho cha ziada ni pesa, dola za Kimarekani ambazo zilikuwa katika kiwango sahihi ambacho kilichokuwa kinaruhusiwa kuingia nacho katika nchi za Ulaya.
Pamoja na matokeo hayo, maafisa wale hawakuwa wameridhika kama Muddy hakuwa mhalifu, wakamchukua na kumpitisha katika mitambo mwingine maalum wakimkagua, wakidhani labda alikuwa amemeza dawa hizo.
Nako pia hawakubainika kama alikuwa amemeza chochote. Pamoja na kulazimishwa kunywa kahawa.
Bado maofisa wale hawakujitosheleza na hatua zote walizokuwa wamezichukua dhidi ya Muddy, walimuingiza katika chumba kingine na kumtaka avue nguo zake zote na kubaki kama alivyotoka tumboni mwa mama yake.
Ulikuwa ni aina fulani ya udhalilishaji ambao Muddy hakuwa amewahi kukutana nao, maafisa wawili wanaume walikuwa wakilisimamia zoezi hilo hatua kwa hatua.
Mkasa mmoja huwa unaanzisha mwingine, baada ya upekuzi wa muda mrefu na kuonekana hakuwa amebeba kitu chochote kibaya, maofisa wale walibaini, Muddy hakuwa na vielelezo vilivyokuwa vinatosheleza kumwonyesha kama alikuwa mwanafunzi anayekwenda kusoma katika chuo kilichokuwapo Uholanzi.
Bahati mbaya ilikuwa upande wake, hakuwa na utambulisho wowote ambao ungeweza kuwaridhisha maafisa wale kukubaliana naye kuhusu safari yake ya kwenda masomoni ya Uholanzi kama alivyokuwa akidai.
Pamoja na Kiingereza chake cha kuombea maji, Muddy alijaribu kujieleza kwa uwezo wake wote lakini maafisa wale hawakuweza kumwelewa hata kidogo.
Muddy alifahamu baadhi ya mambo aliyokuwa akiyazungumza hayakuwa na ukweli, lakini alijitahidi kujitetea na kujenga hoja kadiri alivyoweza ili aweze kuachiwa kuendelea na safari yake.
Alidai alikuwa amepewa msaada na Serikali ya Tanzania kwenda kusoma katika chuo kilichopo Uholanzi.
Hata hivyo, kulikuwa na maswali kutoka kwa maofisa wale ambayo Muddy alishindwa kuyajibu kwa ufasaha na pia alishindwa kuonyesha baadhi ya nyaraka muhimu zilizokuwa zikihusiana na safari yake.
Maafisa wale walipotaka kuiona barua kutoka Serikali ya Tanzania iliyokuwa ikimruhusu kwenda kusoma ilikuwa ni vigumu kwa Muddy kuweza kuitoa barua hiyo.
Pia, maafisa wa uhamiaji walitaka kujua chuo alichokuwa anaenda kusoma, kitu ambacho Muddy hakuwa amejipanga nacho.
Moyoni hapo alimlaumu Fashanu kwa kushindwa kuupanga mpango wake wa safari vizuri. Vilevile maofisa wale walihitaji nyaraka ambazo zingeonyesha uhalali wa yeye kuitwa kwenye chuo hicho.
Halikadhalika Muddy hakuwa na uthibitisho wowote wala hakukijua chuo alichokuwa anaenda kusoma na hakuwa na nyaraka zozote zilizokuwa zikimwonyesha yeye ni mwanafunzi.
Hapo ndipo maafisa walipopata sababu ya kumzuia kuendelea na safari yake, kutokana na kushindwa kuthibitisha uhalali wa safari yake na kumsisitizia alipaswa kurudishwa Tanzania haraka iwezekanavyo.
Hilo lilikuwa pigo kubwa kwake. Pigo lililoivuruga akili yake. Pigo lililokuwa likihatarisha ukamilifu wa ndoto zake.
Hapo Muddy alichanganyikiwa.
Taarifa ya kuzuiwa kuendelea na safari na kurudishwa Tanzania haikupokewa vizuri na Muddy, kitu kilichomfanya machozi yamchuruzike mashavuni mwake.
Jitihada zake za kuwaomba maafisa wale wamuache aweze kuendelea na safari yake zilikuwa zimegonga mwamba.
Maofisa wale walishikilia msimamo wao wa kutaka kumrudisha Tanzania. Muddy hakutaka kabisa kusikia habari za kurudishwa Tanzania.
Pigo la pili kubwa kwake lilikuwa pale ndege aliyopaswa kupanda kuunganisha safari ya kwenda Uholanzi ilipoondoka na kumuacha katika jiji hilo la Stockholm
Hata baada ya ndege hiyo kuondoka, mahojiano kati yake na maafisa wa uhamiaji yaliendelea kwa saa kadhaa na hatimaye ikaamriwa ni lazima arudishwe Tanzania.
Uamuzi huo ulifanyika na Muddy hakutakiwa kuchukua vitu vyake, mizigo na nyaraka zake zilibaki kwa maafisa wale wa uhamiaji kisha yeye akaongozwa moja kwa moja hadi katika chumba kingine kilichokuwa ndani ya uwanja huo wa ndege kusubiri ndege itakayomrudisha Tanzania.
Chumba alichowekwa kilikuwa kikubwa ambacho kilikuwa na viti vingi, huku kukiwa na runinga pande zake zote nne.
Muddy aliketi katika mojawapo ya viti akiwa amejiinamia, taratibu aliona ndoto zake za kutaka kutafuta maisha Ulaya zilikuwa zimeanza kuyeyuka kuanzia hapo.
Katika fikra zake alikuwa akikiona kifungo kikimkabili katika mojawapo kati ya magereza ya Tanzania kwa kosa la kumwibia raia wa kigeni.
Hakutaka kujidanganya, aliamini kesi hiyo ingempeleka kifungoni.
***
Mmoja kati ya wasichana waliokuwa wakifanya shughuli zao katika Uwanja wa Ndege wa Arlanda alimwona Muddy tangu alipochukuliwa na maafisa wa uhamiaji na kufanyiwa mahojiano hadi alipokwenda kuachwa katika chumba kingine kwa ajili ya kusubiri ndege ya kumrudisha Tanzania.
Msichana huyo aliyejulikana kwa jina la Linnie Jonson alifanya udadisi wake na kugundua sababu zilizomfanya abiria huyo kuzuiwa kuendelea na safari yake.
Kutokana na mamlaka aliyokuwa nayo alifika hadi katika chumba alichokuwa amehifadhiwa Muddy kusubiria hatma yake na kuzungumza naye huku akimuuliza baadhi ya maswali.
“Welcome to Stockholm (Karibu Stockholm)…” Linnie alisema huku akichia tabasamu dogo mara baada ya kuingia katika chumba hicho.
“Thank you (Asante)…” alijibu Muddy kama aliyelazimishwa kuzungumza kutokana na fadhaa ambayo hakuwa ameitarajia.
Muddy hakutaka kumchangamkia mwanamke yule kutokana naye kuvaa sare za uhamiaji, aliamini walikuwa ni walewale tu.
Hata Linnie naye aligundua, kijana huyo wa Kiafrika hakuwa tayari kumsikiliza wala kumwamini kwa jinsi alivyokuwa akimtazama.
“Je, unaweza kunieleza tatizo lililojitokeza katika vielelezo vyako?”
Akiwa na hasira huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa kutokana na kutotegemea kilichotokea, Muddy alijitahidi kukielewa Kiingereza cha haraka cha Linnie na akiwa katika hali ya kukata tamaa alijilazimisha kumweleza hakuwa amefanya udanganyifu wowote isipokuwa maofisa wale wa uhamiaji walikuwa wameshindwa kumuelewa.
Hata alipokuwa akizungumza na Linnie, Muddy alionekana kutawaliwa na hofu ya kutotaka kurudishwa Tanzania.
Linnie aliendelea kumdodosa kuhusu safari yake na maisha yake ya Tanzania naye alijitahidi kumuelezea kila kitu kuhusu maisha yake. Mwanamke huyo wa Kizungu alijikuta akivutiwa na maelezo yake na aligundua Muddy hakuwa mtu mbaya.
Linnie alikuwa ametosheka na maelezo ya Muddy akamwambia alikuwa amemaliza zamu yake ya kuwepo kazini uwanjani hapo, hivyo alikuwa anatoka na angerudi jioni.
“Give me a minute… (subiri kidogo) Linnie alisema baada ya mazungumzo hayo mafupi, na kutoka ndani ya chumba hicho.
Muddy ni kama alianza kuwa na imani na mwanamke huyo alimsindikiza kwa macho hadi alipotoka kabisa ndani ya chumba alichokuwamo.
Linnie hakuchukua muda mrefu, ndani ya dakika tano alirudi katika chumba hicho na kukutana tena na Muddy.
Safari hii hakurudi mikono mitupu kama alivyoingia mwanzo, mikononi mwake alikuwa amebeba kikasha kilichokuwa na kikombe kilichojaa chai ya maziwa, mfuko wa nailoni ambao ndani yake ulikuwa umehifadhi sambusa, soseji na vipande vya mikate vilivyopakwa siagi pamoja na mayai mawili ya kuchemsha.
Pia, Linnie alikuwa na chupa ya maji ya kunywa kwa pamoja vitu vyote hivyo alimkabidhi Muddy.
“Najua hali hii si rahisi kwako… naamini unapitia kipindi kigumu,” alisema Linnie wakati akimkabidhi vitu hivyo.
“Asante…” Muddy alishukuru kwa ukarimu aliokuwa amefanyiwa na afisa yule wa uhamiaji.
Kabla ya Muddy hajaanza kula, Linnie alimwambia msaada ambao angeweza kuutoa kumsaidia katika jambo hilo lililomkuta.
“Bahatu mbaya nimemaliza zamu yangu… Naondoka nitarudi jioni, kama nitakukuta nitajaribu kukusaidia…” Linnie alimwambia Muddy aliyekuwa akijiweka tayari kwa ajili ya kunywa chai na vitafunwa alivyoletewa na mwanamke huyo.
“Tafadhali nakuomba kama unaweza kunisaidia nisaidie hata muda huu…” Muddy aliomba huku machozi yakimlengalenga usoni pake kutokana na hofu ya kutokuwa na matumaini ya kuendelea na safari yake.
Mbali ya kuonesha hali hiyo mbele ya Linnie, Muddy, alijitahidi kumueleza mwanamke huyo shida alizokuwa nazo na kuhitaji msaada wa kuendelea na safari yake ili akapate elimu ambayo ingeweza kuwa mkombozi wa familia yake iliyo katika umasikini nchini Tanzania.
“Kwa sasa haiwezekani…sitaweza kufanya kitu chochote nimeshamaliza zamu yangu,” alisisitiza Linnie na kumuaga Muddy aliyekuwa ametawaliwa na unyonge pale alipomuona mwanamke huyo mbichi wa Kizungu akiondoka katika chumba alichokuwamo.
Muddy alizidi kukata tamaa, aliamini mbio za sakafuni zilikuwa zimeishia ukingoni.
Inaendelea…