
Hakuna klabu yoyote ya Afrika Kusini iliyowahi kupindua matokeo ya kufungwa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano kwenye mashindano ya klabu za Afrika.
Hivyo basi, Orlando Pirates ipo katika wakati mgumu wikiendi hii ikiwa inataka kusalia kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pirates iko hatarini kupoteza angalau R10 milioni ikiwa itashindwa kufuzu hatua ya makundi, ambayo ina zawadi ya chini kabisa ya dola za Marekani 700,000, ikilinganishwa na dola 100,000 pekee ambazo itapata endapo itaondolewa hatua ya mtoano.
Pirates ilipoteza vibaya katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili dhidi ya St. Eloi Lupopo ya DR Congo, huko Lubumbashi Jumapili iliyopita na sasa inapaswa kufanya jambo ambalo hakuna klabu ya Afrika Kusini iliyowahi kufanya, yaani kupindua matokeo ya kufungwa 3-0.
Hii ilikuwa ni mara ya saba kwa klabu ya Afrika Kusini kufungwa kwa tofauti ya mabao matatu au zaidi ugenini katika mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano ya mashindano ya klabu barani Afrika.
Kaizer Chiefs ilifungwa 4-0 na Espérance ya Tunisia katika raundi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2005 na ikaondolewa baada ya kushinda 2-1 mechi ya marudiano.
Katika mashindano hayo hayo mwaka 2014, Chiefs ilifungwa 3-0 na AS Vita Club ya DR Congo, jijini Kinshasa na ikashindwa kugeuza matokeo nyumbani, ingawa ilikaribia baada ya kushinda 2-0.
Cape Town City nayo ilifungwa 3-0 nyumbani katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2022-2023 dhidi ya Petro Atlético ya Angola kisha ikapoteza tena 1-0 ugenini, jijini Luanda.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2005, SuperSport United ilifungwa 4-1 na Dolphins ya Nigeria katika mechi ya kwanza ya raundi ya nne na kuambulia sare ya 2-2 nyumbani ziliporudiana.
Katika mashindano hayo hayo mwaka 2016, Bidvest Wits ilienda Tanzania na kikosi cha wachezaji wa akiba dhidi ya Azam FC na ikapoteza kwa mabao 3-0, kisha ikafungwa tena 4-3 nyumbani.
Jomo Cosmos ilifungwa 3-0 na Mansoura ya Misri ugenini katika robo fainali ya Kombe la Washindi wa Afrika mwaka 1997 na ikatoka sare ya 2-2 nyumbani na kuondolewa.
Hata hivyo, kumekuwa na matukio kwa klabu za Afrika Kusini zimeweza kugeuza matokeo ya kufungwa kwa tofauti ya mabao mawili, kama ilivyotokea mwaka 2005 pale SuperSport United ilipokutana na FC Lupopo katika Kombe la Shirikisho. Wakati huo, Lupopo ilishinda 2-0 nyumbani Lubumbashi, lakini SuperSport walishinda 2-0 katika marudiano na kusonga mbele kwa mikwaju ya penalti.
Klabu nyingine kama Black Leopards, Santos, na Mamelodi Sundowns pia zimewahi kugeuza matokeo ya kufungwa kwa mabao 2-0 na kushinda hatua za mtoano katika miaka michache iliyopita.
Je Orlando itatoboa vipi ikirudiana na FC Lupopo wikiendi hii? Tusubiri tuone!