
-
- Author, Mungai Ngige
- Nafasi, BBC Global Disinformation Unit
- Author, Lamees Altalebi and Ahmed Nour
- Nafasi, BBC Arabic Forensics
- Author, Fardowsa Hanshi
- Nafasi, BBC Africa
Uchunguzi wa BBC umebaini kuwa kuna makumi ya akaunti za mitandao ya kijamii za watu wanaojifanya kuwa wanamitindo na watu maarufu Waislamu na Wasomali, lakini zinatumika kueneza propaganda za kisiasa na kijeshi.
Mwanamke mmoja anaonekana kwenye picha akiwa na tabasamu na amevaa buibui ya buluu. Picha yake imetumika kwenye mitandao ya X, TikTok na Facebook, na mara kwa mara akaunti hizo huchapisha maudhui yanayosifia nchi ya Somalia.
Hata hivyo, BBC ilipowasiliana na mwanamke huyo ambaye ni mshawishi wa mitindo ya maisha mtandaoni alishangazwa na matumizi hayo ya picha zake. Alisema:
“Si mimi. Picha zangu zinatumika bila idhini yangu, na siwezi kufanya lolote dhidi ya hawa watu wanaojifanya kuwa mimi.”
Yeye ni mmoja kati ya wanawake kadhaa ambao picha zao zimetumiwa bila ruhusa kueneza maudhui yenye mwelekeo wa kisiasa yanayohusiana na Somalia, Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kitengo cha BBC Global Disinformation Unit & Forensics cha Idhaa ya Kiarabu kimetambua zaidi ya akaunti 100 zinazohusiana na mtandao huo wa propaganda.
Haijabainika wazi ni nani anasimamia operesheni hiyo, lakini maudhui mengi yanaisifu UAE na yanaendana na malengo ya sera yake ya kigeni.
UAE na ushawishi Afrika Mashariki
UAE imekuwa na ushawishi mkubwa katika Afrika Mashariki, ikifanya uwekezaji mkubwa katika sekta za usalama na miundombinu ya baharini, hasa katika maeneo ya Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, maeneo ya kimkakati ambapo Somalia ipo.
Akaunti nyingi zinazoonekana kuwa bandia pia zinaunga mkono kikundi cha wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) ambacho kinapigana na jeshi la Sudan katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Jeshi la Sudan limeishutumu Abu Dhabi kwa kuwasaidia RSF kwa silaha na fedha madai ambayo UAE imekanusha mara kadhaa.
Mbinu zilizotumika kueneza propaganda

Chanzo cha picha, Unknown / Shared on X
Kwa kutumia zana za uchambuzi wa mitandao ya kijamii, BBC ilibaini kuwa kati ya Januari 2023 hadi Septemba 2025, akaunti 111 za X (zamani Twitter) zilichapisha zaidi ya machapisho 47,000 yaliyopata jumla ya likes 300,000 na kufikia zaidi ya watu milioni 215.
Akaunti hizo zilifunguliwa ndani ya muda mfupi, zilibadilisha majina ili kuepuka kugunduliwa, zilitumia picha zilizotengenezwa kwa teknolojia ya akili bandia (AI), na zilichapisha maudhui yanayofanana kwa lugha tofauti.
Tabia hizi zote zinaashiria kuwa kulikuwa na juhudi za kisasa za ushawishi zisizo za kweli.
Baadhi ya akaunti kama hizo pia zilibainika kwenye TikTok na Facebook, zikichapisha maudhui sawia.
Kuwalenga Wasomali
Akaunti nyingi zilijifanya kuwa ni za Wasomali walioko ndani au nje ya Somalia, zikisifu serikali ya Somalia, jeshi lake, watu wake na uzuri wa nchi kwa ujumla.
Zilitumia majina ya koo za Kisomali kama Isaaq, Ogaden, Ajuran, Dir, Digil, Darod na Akisho, ili kujenga imani kwa watumiaji wa mitandao wa Kisomali.
BBC ilitumia teknolojia ya kutafuta picha mtandaoni (reverse image search) na kubaini kuwa baadhi ya picha hizo ni za wanamitindo halisi au washiriki wa mashindano ya urembo walioweka picha zao kwenye mitandao mingine.
Mmoja wao, mshindi wa zamani wa taji la urembo, alisema hajawahi kuwa na akaunti ya Facebook na hakujua picha zake zinatumiwa kutangaza serikali ya Somalia.
Picha hiyo ilitumika kwenye akaunti iliyokuwa ikijitambulisha kama “Halima,” ambayo baadaye ilibadilika jina na kuwa kama tovuti ya habari kwa lugha ya Kiarabu.
Kampuni ya Meta ilisema ilikuwa inachunguza tabia ya akaunti hiyo kwa kushukiwa kuwa ya uongo.

Chanzo cha picha, Reuters
Wanawake wengine wanne pia walithibitisha kuwa picha zao zinatumiwa bila idhini yao.
Mama wa mmoja wao alisema binti yake hana akaunti ya X na hajui chochote kuhusu mtandao unaotumia picha zake.
Mwingine, mwanamitindo wa Marekani, alitoa taarifa kupitia meneja wake kuwa walihuzunishwa sana kugundua kuwa picha zake zinatumiwa kwenye akaunti ya TikTok bila ruhusa.
TikTok ilithibitisha kuwa akaunti hiyo na nyingine kadhaa zilifutwa kwa kukiuka sera za jukwaa kuhusu shughuli za ushawishi wa siri na akaunti za kuiga.
“Tuna timu maalum zinazofanya kazi kwa saa zote kuhakikisha usalama na kuzuia tabia za kudanganya kwenye jukwaa letu,” msemaji wa TikTok alisema.
Dkt. Marc Owen Jones, mtaalamu wa habari za uongo kutoka Chuo Kikuu cha Northwestern, Qatar, alisema kuwa akaunti hizo ni “sock puppets” — yaani akaunti feki zinazoundwa kwa lengo la kueneza mtazamo fulani huku zikificha watu walio nyuma yake.
Akaunti hizo zilitumia lugha ya Kisomali, Kiingereza na Kiarabu cha kisasa (fasihi), lugha isiyotumika sana mitandaoni na vijana wanaozungumza Kiarabu jambo linaloashiria kuwa huenda walengwa wa maudhui hayo hawakuwa raia wa kawaida.
Majukwaa ya mitandao ya kijamii yalisema watumiaji waliodhulumiwa wanaweza kuripoti akaunti hizo moja kwa moja.
X (zamani Twitter) haikutoa maoni kuhusu iwapo akaunti hizo zilikiuka sera zake.
Kuelekea Sudan
Kwa muda fulani, akaunti hizo zilianza kuandika kuhusu vita vya Sudan, zikitumia picha zilizoboreshwa na AI na jumbe zilizorudiwa mara kwa mara.
Mnamo Agosti, baadhi ya akaunti zilidai kuwa jeshi la Sudan liliwaua raia 27 na kuwazika katika eneo la Al Obeid, Sudan Kusini.
BBC haikuweza kuthibitisha madai hayo kutoka vyanzo huru, na shirika la ukaguzi wa taarifa Beam Reports lilisema halikuweza kupata ushahidi wa kuthibitisha habari hizo.
Madai hayo yalionekana kuwa jibu kwa ripoti za televisheni ya Sudan inayounga mkono jeshi, kwamba ndege ya UAE iliyobeba mamluki wa Colombia ilishambuliwa na ndege za kivita. Takriban watu 40 waliuawa.
Kwa kueneza habari tofauti, akaunti hizo zilionekana kusaidia simulizi zinazounga wanamgambo wa RSF, kundi la wanamgambo ambalo limekuwa katika vita na jeshi la Sudan tangu Aprili 2023.
Kwa kurudisha nyuma, akaunti zilikuwa zikitumiwa kukuza masimulizi ambayo yangeonekana kuendana na RSF na UAE.
UAE daima imekuwa ikikanusha shutuma kwamba inaunga mkono RSF au inaunga mkono mamluki wa kigeni wanaopigana pamoja nayo.

Chanzo cha picha, Reuters
Ni nani atazisimamia?
Haijajulikana wazi ni nani anayesimamia mtandao huu wa akaunti, lakini maudhui mengi yanayohusu Somalia na UAE yanaonekana kuelemea upande wa sera ya kigeni ya UAE.
Kwa mtazamo wa kwanza, kimsingi wanaisifu Somalia na mara nyingi serikali yake ikiwa na asilimia 40 ya machapisho yanayotaja Somalia moja kwa moja.
Dkt. Jones alisema:
“Wanaotengeneza akaunti hizi hujifanya vijana warembo kutoka nchi ambazo UAE ina maslahi. Kuna kundi la Somalia, lakini pia nimeshuhudia kundi la Mauritania, Algeria na Morocco.”
Aliongeza kuwa kuna mchanganyiko wa siasa na biashara, na mada zinazotangazwa hutegemea maslahi ya UAE katika kila nchi.
Baadhi ya akaunti zilionyesha picha za misaada ya chakula kutoka UAE zikiwa na ujumbe kama “UAE yaunga mkono Somalia.”
Hata hivyo, uhusiano huu wa kiuchumi umekuwa na migogoro, hasa kutokana na baadhi ya Wasomali kupinga msaada wa UAE kwa maeneo kama Somaliland, Puntland na Jubaland, maeneo yaliyojitangaza kuwa na mamlaka huru.
UAE pia imesaidia mafunzo ya kijeshi na ufadhili wa operesheni dhidi ya Al Shabaab na vikundi vya kigaidi.
Kulingana na Alessandro Accorsi, mchambuzi huru wa habari za upotoshaji ambaye anabobea katika Mashariki ya Kati, ni vigumu kubandika kampeni zinazounga mkono masimulizi ya sera ya kigeni ya UAE kwa jimbo kwa sababu mfumo wa ushawishi wa Abu Dhabi unategemea idadi kubwa ya makampuni ya PR.
“Ni vigumu kuwa na maelezo ya moja kwa moja kwa sababu mara nyingi ni makampuni ya kujitangaza na kushawishi makampuni ya uendeshaji ambayo yanaweza kuwa na kandarasi na mtu binafsi,” alisema.
Serikali za UAE na Somalia hazikujibu maswali ya BBC.
Uchanganuzi wa maudhui pekee hauelezi kina cha nani anaongoza akaunti hizi na ni vigumu kwa wanawake kujua ni nani aliyepiga picha zao.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi