Mabao 43 yalifungwa katika michezo 9, huku timu sita zikifunga magoli zaidi ya manne kwenye usiku wa Oktoba 21 utakaokumbukwa kama usiku uliokuwa na mabao mengi kabisa katika msimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
PSV Eindhoven iliichapa Napoli ya Italia mabao 6-2, huku Arsenal na Inter Milan pia zikiondoka na ushindi mnono na kujiimarisha zaidi kwenye nafasi za juu za ligi hiyo barani Ulaya.
PSG, mabingwa watetezi, inaongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya siku ya Jumanne kuitandika Bayer Leverkusen ya Ujerumani7-2, katika mechi ambako kulishuhudiwa timu zote zikiwa na wachezaji 10 hata kabla ya nusu ya pili ya mchezo.
Magoli mawili ya Desire Doue yaliiweka kwenye nafasi nzuri zaidi mabingwa hao watetezi ya kuudhibiti mchezo na mambo yalizidi kuwanyookea baada ya mapumziko, wakati Nuno Mendes alioongeza bao dakika tano tu baada ya kurejea uwanjani
Ousmane Dembele ambaye aliingia akitokea “benchi” baada ya kuwa majeruhi aliiongezea nguvu PSG baada ya kufunga dakika ya 66. “Hiyo ni michezo mitatu, ushindi mara tatu na tunaongoza msimamo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya” alisema Dembele. Tumeanza kampeni vizuri sana na hasa kwa kuzingatia ugumu uliokuwepo msimu uliopita.
Rashford aendelea kuipaisha Barcelona
Barcelona nayo iliifunga Olympiakos 6-1, ikirejea kutoka kwenye majeraha ya kufungwa na PSG ligi hiyo ilipoanza mwezi uliopita. Fermin Lopez aliifungia timu yake ‘hat trick’ na Marcus Rashford akifunga mabao mawili dhidi ya Olympiakos iliyokuwa na wachezaji 10.
Barcelona ilitumia mwanya huo baada ya Santiago Hezze kuonyeshwa kadi nyekundu katika nusu ya pili ya mchezo kufunga mabao manne na kumaliza mchezo wakiwa na jumla ya mabao 6.
Rashford anayekipiga Barca kwa mkopo kutoka Manchester United, sasa ana mabao manne katika michezo mitatu kwenye msimu huu wa Champions. “Mara nyingine ni ngumu kumpiku mpinzani wako, lakini tuna wachezaji wenye uwezo wa kufunga kwenye maeneo mengi, kwa hiyo kufunga sio tatito kwetu,” alisema Rashford.
Arsenal yaizidi nguvu Atletico
Arsenal, vinara wa Ligi ya England waliiitandika Atletico Madrid 4-0, huku Viktor Gyokeres akifunga magoli mawili. Inter Milan washindi wa pili wa Champions msimu uliopita pia iliifunga Union Saint-Gilloise 4-0.
Arsenal inayoongoza Ligi ya Premier inaonekana imara pia kwenye Champions. Kikosi hicho cha Mikel Arteta kiliizidi nguvu Atletico Madrid kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Emirates, huku mshambuiliaji Gyokeres aliyesaini na kikosi hicho majira ya joto akiukamilisha ushindi kwa mabao mawili katika kipindi cha dakika tatu.
“Nimefurahi, kwa kweli anastahili. mchango wake kwenye timu ni mkubwa. tunathamini mengi anayoyafanya kwa ajili ya timu na nimeona tabasamu usoni mwake leo,” alisema Arteta alipomzungumzia Gyokeres ambaye hajafunga goli hata moja kwenye mechi saba zilizopita. Arsenal sasa ni ya tatu, ikitanguliwa na PSG na Inter Milan, kwa tofauti ya magoli.
Halaand hashikiki
Goli la Haaland liliisaidia Manchester City kuondoka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Villareal na amezidi kupaa kwenye michuano hiyo. Raia huyo wa Norway hadi sasa amefunga mabao 24 katika mechi 14 msimu huu. Amefunga mabao katika mechi 12 mfululizo. Sasa ana mabao 53 kwenye Ligi ya Champions, baada ya kucheza mechi 51 tu.
Mchezo mmoja tu ambao hakufunga ulikuwa ni dhidi ya Totanham Hotspurs, iliyowalaza 2-0 mwezo Agosti. Bernado Silva pia ameendelea kuonyesha makucha, wakati City ikipanda hadi nafasi ya 5 ya Ligi ya Champions.
Napoli yashangazwa, Dortmund yashinda
Napoli hawakuamini macho yao walipojikuta wanalazwa chali na PSV. Kikosi hicho cha Antonio Conte kimeendelea kupoteza mechi baada ya siku ya Jumamosi pia kufungwa 1-0. Napoli imeshinda mara moja tu kati ya michezo mitatu ya Ulaya hadi sasa.
Harvey Barnes alifunga mabao mawili na kuisaidia Newcastle kuondoka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Benfica huku Borussia Dortmund ikiondoka na ushindi mnono wa 4-2 dhidi ya Copenhagen.