Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kutekeleza kwa mafanikio Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET – Project), wenye lengo la kuibadilisha elimu ya juu nchini kuwa injini ya maendeleo ya kiuchumi.
Mradi huu wa miaka mitano (2021/2022–2025/2026), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, umeelekeza nguvu zake katika vyuo vikuu 14 vilivyopo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kikiwemo Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) na taasisi tano zilizopo chini ya Wizara ya Fedha, MUCE imetengewa kiasi cha Dola za Kimarekani milioni nane, sawa na Sh 18.62 bilioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu, kuboresha mitaala, kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji, kuendeleza rasilimaliwatu, kuimarisha elimu jumuishi na usawa wa kijinsia, kukuza tafiti tumizi, pamoja na kuanzisha na kuboresha majukwaa ya ufundishaji kwa njia ya mtandao na kidijitali. Lengo lingine muhimu ni kuboresha uhusiano na sekta binafsi na tasnia.
Matokeo ya uwekezaji huu mkubwa wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha elimu ya juu inatoa mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya Taifa na kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa kuzingatia vipaumbele vya mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.
Rasi wa Chuo hicho, Profesa Method Semiono akizungumzia mradi huo amesema “Kwa kweli ninaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuridhia mradi huu kutekelezwa katika chuo chetu kwani ndiyo msingi wa maboresho ya elimu ya juu nchini. Mradi huu unaonesha nia ya dhati ya Serikali kutimiza ahadi yake kwa wananchi ya kuboresha mfumo wa elimu nchini ili kuwaletea watu wake maendeleo.”
Utekelezaji wa mradi wa HEET MUCE
MUCE ilianza rasmi kutekeleza Mradi wa HEET Septemba 2021 na mradi unatarajiwa kukamilika Juni 2026. Katika ujenzi wa miundombinu, chuo kimepewa Sh 14.8 bilioni ili kujenga majengo manne, ambayo ni jengo la hosteli za wanafunzi, jengo la maabara ya fizikia, jengo la midia anuwai na elimu maalum na jengo la Sayansi. Ujenzi wa majengo haya utaongeza uwezo wa chuo kudahili wanafunzi utaongezeka kwa wanafunzi zaidi ya elfu nne.
Uboreshaji wa mitaala
Serikali kupitia mradi wa HEET imewezesha MUCE kufanya mapitio ya mitaala ya programu tano (5) na kuanzisha mitaala mipya 30 katika fani mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sayansi, teknolojia na elimu.
Jengo la sayansi linaloendelea kujengwa chini ya mradi wa HEET unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo Iringa.
Mitaala hii imeandaliwa kwa kushirikisha tasnia husika ili kuhakikisha kuwa wahitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika na soko la ajira na wenye uwezo wa kujiajiri na kuajirika. Aidha, mitaala hiyo imezingatia masuala muhimu yaliyopo katika jamii kwa sasa kama vile akili mnemba, elimu ya masuala ya fedha na mengineyo.
Katika eneo hili la uboreshaji wa mitaala, chuo kimewezeshwa kuandaa programu saba za umahiri na mbili za uzamivu katika fani mbalimbali na hivyo kukifanya Chuo kuwa na programu za kwanza za shahada za uzamivu zilizoanza kufundishwa mwaka wa masomo 2024/2025. Kuongezeka kwa programu hizi, kumekisaidia chuo kufikisha jumla ya programu za uzamili 14 kutoka programu tano zilizokuwepo awali.
Matumizi ya TEHAMA na dijitali katika ufundishaji na ujifunzaji
Ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa programu chuoni, kupitia mradi wa HEET, chuo kinafanya mageuzi makubwa katika mifumo ya TEHAMA na matumizi ya digitali. Chuo kinafanya ukarabati mkubwa wa mifumo ya TEHAMA na kutandaza fibre ya kusambaza mtandao Chuoni ili kuboresha upatikanaji wa mtandao wa intaneti. Pia, ujazo ya mtandao wa intaneti umeongezwa na kufanya mtandao huo kuwa wa kasi na uhakika.
Ili kuwezesha ufundishaji wa programu mpya na matumizi ya mbinu za kisasa za ufundishaji, watumishi wa Chuo wamejengewa uwezo kwa kuwezeshwa kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu.
Kwa upande wa mafunzo ya muda mfupi, watumishi wa Chuo wamewezeshwa kuhudhuria mafunzo ya mbinu za kisasa na bora za ufundishaji, utayarishaji wa masomo kwa njia ya kidigitali na mtandao, na uzingatiaji wa watu wenye mahitaji maalumu katika ufundishaji.
Kwa upande wa mafunzo ya muda mrefu, wafanyakazi 31 wamewezeshwa kuhudhuria mafunzo ya Shahada za Uzamili katika vyuo bora ndani na nje ya nchi. Watumishi hawa wameshaanza kuhitimu na kurejea Chuoni kutekeleza majukumu yao. Akizungumzia faida za Mradi huu, mmoja wa watumishi waliofaidika na kusomeshwa, Dk Baraka Luvanga anasema, “Kwa hakika mradi wa HEET umenipa fursa ya kujengewa uwezo katika maeneo yangu ya ubobezi. Ninaishukuru sana Serikali kwa kufikiria kuja na mradi huu.”
Ushirikiano na sekta binafsi na tasnia
Kupitia mradi wa HEET, MUCE imefanikiwa kuboresha mahusiano yake na sekta binafsi na tasnia. Kupitia Kamati ya Ushauri wa Viwanda, chuo kimeweza kupata ya namna ya kuandaa mitaala inayozingatia mahitaji ya soko. Vilevile, kupitia mahusiano hayo, wanafunzi wamepata fursa za kufanya mafunzo kwa vitendo katika sekta hizo. Ili kuimarisha mahusiano hayo, Chuo kimesaini mikataba 16 ya makubaliano na taasisi mbalimbali katika tasnia.
Kwa mfano, mahusiano baina ya chuo na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA) pamoja na Sao Hill Industries yanakiwezesha chuo kuimarisha uwezo wa utafiti na utoaji wa elimu katika fani ya mimea na mazao yake.
Akizungumzia mashirikiano baina ya MUCE na tasnia, Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru anasema, “kwa kweli Serikali inastahili pongezi katika eneo hili la kuimarisha mahusiano ya vyuo na tasnia kwani imevifanya vyuo kuwa na mchango wa moja kwa moja katika Taifa na kupunguza malalamiko ya wadau kuwa vyuo vinatoa wahitimu wasiokidhi mahitaji ya soko.”
Uhusiano na Dira ya Taifa
Mradi wa HEET una mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kujenga rasilimali watu yenye ubunifu, ujuzi na uwezo wa kuchochea uchumi wa kati. Vilevile, Mradi huu unaendana na Ilani ya chama tawala cha CCM (2025–2030) na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023, zinazosisitiza elimu ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama msingi wa maendeleo. Katika muktadha huo, MUCE imepata fursa ya kuchangia moja kwa moja kwenye ajenda ya Taifa ya kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mabadiliko ya sasa ya sayansi na teknolojia.
Manufaa ya mradi wa HEET kwa wanafunzi
Kupitia Mradi wa HEET, wanafunzi wa MUCE wamepata manufaa ya moja kwa moja kwa kuwezeshwa kupata vifaa vya kujifunzia, kuboreshwa kwa mazingira yao ya kujifunzia na kupewa mafunzo na semina mbalimbali. Mwanafunzi Magreth Mwaijande anasema, “Kwa mara ya kwanza tunasoma katika mazingira ya kisasa kabisa maabara, madarasa na vifaa vya kidijitali vimeboreshwa kwa kiwango cha juu.”
Naye Mwanafunzi Rehema Msigwa anaongeza, “Jengo jipya la Midia Anuwai na Elimu Maalum limetupatia fursa ya kusoma bila vikwazo vya kimazingira.” Kupitia uwekezaji huu uliochagizwa na Mradi wa HEET, MUCE sasa inatambulika kama kitovu cha elimu jumuishi Tanzania.
Mradi wa HEET umeibadilisha MUCE kuwa taasisi ya kisasa, yenye mitaala inayoendana na soko, wahadhiri wenye ujuzi na weledi mkubwa, na wanafunzi wanaojifunza wenye umahiri unaoendana na mahitaji ya sasa.