
Makamu Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania Bara John Heche, amekamatwa na polisi Jumatano asubuhi jijini Dar es salaam, wakati akiingia kwenye lango la Mahakama kuu, kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wake Tundu Lissu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Chama hicho kinasema , haijafahamika ni kwanini Heche amekamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Kati.
Hii inakuja baada ya Jumamosi, Oktoba 18, 2025 uongozi wa Chadema kueleza kuwa kiongozi huyo alizuiwa na maafisa wa uhamiaji kwenda nchini Kenya, kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Idara ya uhamiaji, nchini humo nayo ilidai kuwa, kiongozi huyo wa upinzani alikuwa amevuka mpaka na kwenda nje ya nchi kinyume cha utaratibu, madai ambayo CHADEMA imekanusha.
Haya yanajiri, kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, ambao chama hicho cha upinzani, hakitashiriki baada ya kuzuiwa na Tume ya uchaguzi, kwa kutosaini maadili ya uchaguzi. Chama hicho kinataka mageuzi ya sheria za uchaguzi kabla haujafanyika.
Katika hatua nyingine, Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, limelaani kile inachotaja kuwa “wimbi la hofu na ukandamizaji” nchini Tanzania kutokana na kukamatwa, kupotezwa kwa wapinzani na wanaharakati.