KWA kinachofanywa na Morice Abraham ndani ya kikosi cha Simba bila shaka Elie Mpanzu, Jean Charles Ahoua, Kibu Denis na Neo Maema wakizubaa tu imekula kwao.
Unajua kwa nini? Kuna wakati nyota mpya huibuka kimyakimya, bila ya kelele nyingi, lakini ghafla inapochomoza, kila anayetazama anabaki na mshangao mkubwa, huo ndio ukweli unaoonekana sasa ndani ya Simba kupitia Morice Abraham, mchezaji ambaye amegeuka kuwa kipenzi cha wekundu wa Msimbazi.
Kiungo huyo amesajiliwa na Simba msimu huu baada ya kuachana na FK Spartak Subotica ya Serbia. Usajili wake haukuwa na mbwembwe nyingi tofauti na ilivyokuwa kwa wachezaji wengine kama Mohammed Bajaber, Neo Maema na Jonathan Sowah.
Lakini kwa sasa, jina lake limeanza kupenya midomoni kwa wengi baada ya kuuwasha ndani ya Simba, akitajwa kama mchezaji tegemeo sambamba na nyota wengine akiwamo Elie Mpanzu na Jean Charles Ahoua ambao wamekuwa wakifanya vizuri kwenye kikosi hicho tangu msimu uliopita wakiwa chini ya kocha Fadlu Davids.
Kuondoka kwa Fadlu na kuja Dimitar Pantev, Morice ndiyo kwanza ameendelea kufanya vizuri kila anapopata nafasi ya kucheza.

Wakati mashabiki wengi walikuwa wakizungumzia wachezaji wenye majina makubwa waliozoeleka, Seleman Matola ndiye mtu wa kwanza kabla ya Pantev aliyekuwa akimwangalia kiungo huyo kwa jicho la tofauti na ndio maana alimpa nafasi katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara wakati akikaimu nafasi ya kocha mkuu pindi tu Fadlu alipotimkia Raja Casablanca.
Ndani ya mechi mbili za ligi, Morice ametumika kwa dakika 114, aliingia katika mechi ya kwanza ambayo Simba ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate akichukua nafasi ya Kibu na kushambulia akitokea pembeni kwa dakika 45 za kipindi cha pili.
Kiwango kizuri alichoonyesha kilimfanya Matola kumpa nafasi ya kuanza katika mechi iliyofuata dhidi ya Namungo, akacheza kwa dakika 69 na kuiwezesha Simba kushinda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa.
PANTEV AKUBALI MZIKI
Kwa mujibu wa Pantev, mchezaji huyo ana vitu vitatu vinavyomtofautisha na wengine ambavyo ni uwezo wa kukaa na mpira, kufanya uamuzi kwa wakati na kushirikiana kwa uelewano mkubwa na wachezaji wenzake.

Pantev amesema: “Morice ana kipaji asilia na nililigundua hilo ndani ya kipindi kifupi. Anafanya uamuzi ndani ya sekunde chache kitu ambacho kinarahisisha kufanya mashambulizi kwa haraka.”
Bao la tatu la Simba dhidi ya Nsingizini Hotspurs wikiendi iliyopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika, lilikuwa ni matunda ya kile ambacho Morice anaweza kufanya. Pasi yake ya haraka akiwa katikati ya uwanja kwenda kwa Kibu Denis, ilionekana ni ya kiwango kikubwa, Kibu akafunga kwa utulivu.
MORICE KWENYE MFUMO
Simba ya Pantev imekuwa ikicheza soka la kasi, ndani ya falsafa hiyo, Morice ameonekana kuwa anaweza kuongeza kitu tofauti. Uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja kama namba 10, winga wa kulia au kushoto unampa kocha chaguo pana la mbinu za ushambuliaji.
Viungo wengine wa eneo la ushambuliaji wenye kasi ni Kibu na Mpanzu, tofauti na Ahoua ambaye amekuwa si mchezaji mwenye kasi, hii inaweza kumfanya Morice taratibu kumtoa kiungo huyo kikosini. Kumbuka Ahoua msimu uliopita alikuwa mchezaji mwenye mchango mkubwa kwenye kikosi cha Simba akimaliza kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akifunga 16, huku akitoa asisti tisa. Katika mazoezi, Pantev amekuwa akimtumia Morice kama sehemu ya majaribio ya mifumo tofauti huku ule mfumo wake maalum ukiwa ni 4-3-3.

WASIKIE WADAU
Wadau mbalimbali wa soka nchini wameeleza vile nyota huyo anaweza kuwa lulu kwenye kikosi hicho kama ataendelea kujituma na kufanyia kazi maelekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo.
Nyota wa zamani wa Kagera Sugar, George Kavila anasema: “Ana utulivu, anapiga pasi zenye macho na ana kasi ambayo inaweza kumkumbusha mtu enzi za Emmanuel Okwi.”
Kavila anaamini Morice anaweza kuwa mrithi sahihi wa Clatous Chama katika eneo la ubunifu ambaye kwa sasa yupo Singida Black Stars.
“Kama ataendelea hivi, Simba haina haja ya kumtafuta mbunifu mwingine. Ana ubongo safi wa soka na anaelewa mpangilio wa timu,” ameongeza.
Pamoja na sifa hizo, wataalamu wengine wameeleza kuwa kijana huyo anapaswa kulindwa kisoka apewe muda, apate mwendelezo na asibebeshwe mzigo wa matarajio makubwa mapema.

“Anaweza kuwa nyota mkubwa, lakini ni muhimu aendelee kuimarika bila presha,” amesema kocha wa zamani wa Gwambina na Mtibwa Sugar, Mohammed Badru.
Morice mwenyewe anasema anajisikia fahari kuvaa jezi ya Simba na kuona ndoto yake ikiendelea kukua.
“Nilipofika hapa, nilijua ninakuja kwenye klabu yenye historia kubwa. Lakini pia nilijua lazima nijitume mara mbili zaidi. Kocha amenipa imani, nami siwezi kumwangusha,” amesema Morice.
“Nataka kuona Simba inafika mbali Afrika, nataka kushinda mataji na zaidi ya yote, nataka kuacha alama. Hii ni klabu ya mamilioni ya watu, lazima nishindane kwa ajili yao.”