Tukio hilo limetokea siku moja tu baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuahirisha mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika kati yake na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akisema hataki kushiriki katika kile alichoita “mkutano wa kupoteza muda.” 

Waziri wa Nishati wa Ukraine Svitlana Grynchuk, amesema mashambulizi makubwa ya Urusi dhidi ya Ukraine yaliyofanyika usiku kucha yaliendelea hadi mapema Jumatano.

Tymur Tkachenko ambaye ni afisa wa ngazi ya juu katika utawala wa Kiev amesema mashambulizi hayo ni juhudi za hivi karibuni zaidi za Urusi kusambaratisha mfumo wa nishati wa Ukraine kabla ya kuanza kwa msimu wa baridi. Kulingana na Tkachenko, watu wasiopungua 18 walijeruhiwa kwenye mashambulizi hayo.

Wizara ya nishati ya Ukraine imesema mashambulizi hayo yalisababisha umeme kukatika kote Ukraine, lakini tayari wameanza kufanya ukarabati ili kurejesha umeme haraka iwezekanavyo.

Mashambulizi makali ya Urusi yamejiri siku moja tu baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusitisha mkutano uliokuwa ukipangwa kufanyika kati yake na Rais Vladimir Putin mjini Budapest Hungary akisema hataki mkutano wa kupoteza wakati.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Allison Robbert/UPI Photo/Newscom/picture alliance

“La hasha. Sitaki kuwa na mkutano wa kupoteza muda. Sitaki kupoteza muda. Kwahivyo nitaona kile kitakachofanyika. Lakini tumefanikisha makubaliano mengi mazuri. Yote ni mikataba ya amani, na  makubaliano thabiti. Lakini kwa hili niliambia kila upande kujiondoa katika mstari wa mapambano na warudi nyumbani… Kwa hivyo tutaona kitakachojiri. Hatujafikia maamuzi yoyote.”

Shinikizo kwa Urusi

Kupitia taarifa, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema masaibu ya usiku huo ni ishara nyingine kwamba Urusi haihisi shinikizo lolote dhidi ya kurefusha mzozo wake na Ukraine.

Zelensky amesema mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu wa miji mingi ikiwemo Kiev, Zaporizhzhia, Odesa, Chernihiv, Dnipropetrovsk, Kirovohrad, Poltava, Vinnytsia, Zaporizhzhia, na maeneo kadhaa ya majimbo ya Kyiv, Cherkasy, na Sumy.

Ukraine Lutsk 2016 | Ndege ya kivita ya Ukraine Su-24 wakati wa luteka ya kijeshi
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ataka washirika wa Ukraine kuchukua hatua zaidi dhidi ya Urusi kutokana na mashambulizi yakePicha: Giovanni Colla/Stocktrek Images/picture alliance

Zelensky ameuhimiza Umoja wa Ulaya, Marekani na nchi zilizoendelea zaidi kiviwanda katika kundi la G7, kuchukua hatua za kuiwekea Urusi vikwazo zaidi.

‘’Ni muhimu ulimwengu usifyate mdomo sasa, bali ipo haja ya kutoa jibu la pamoja dhidi ya mashambulizi hatari ya Urusi,” amesema Zelensky kwenye taarifa yake.

Katika tukio jingine, Jenerali wa jeshi la Ukraine amesema vikosi vya nchi yake vimeshambulia kiwanda cha kemikali cha Urusi kilichoko Bryansk usiku wa kuamkia leo Jumatano, kwa kutumia makombora aina ya Storm Shadow.

Kiwanda hicho ni muhimu kwa majeshi ya Urusi kwani hutengeneza vilipuzi, baruti, mafuta ya makombora na risasi vinavyotumiwa katika mashambulizi ya mara kwa mara.

(APE,RTRE)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *