Mkutano wa Nne wa Kistratijia wa “Iran na Eurasia; Biashara, Diplomasia na Utaratibu Mpya wa Kikanda,” umefanyika leo katika Kituo cha Mikutano cha Shirika la Utangazaji la Sauti na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Tehran.

Lengo kuu la mkutano huo uliohudhuriwa na watunga sera, wanaharakati wa sekta binafsi, mashirika yanayolenga mauzo ya nje, makampuni mbalimbali, wasomi na wataalamu watajika ni kuchunguza vipengele vya utekelezaji wa makubaliano ya biashara huria kati ya Iran na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.

Mkutano wa Nne wa Kistatejiai wa Iran na Eurasia; Biashara, Diplomasia na Utaratibu Mpya wa Kikanda unahesabiwa kuwa tukio muhimu na lenye taathira kubwa katika njia ya maingiliano ya kiuchumi na kisiasa kati ya Iran na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.

Kuelezea fursa zinazotokana na utekelezaji rasmi wa Makubaliano ya Biashara Huria ya Umoja wa Kiuchumi wa Iran na Eurasia, ambayo yametayarisha jukwaa muhimu kwa ajili ya kustawisha ushirikiano katika sketa ya usafirishaji na lojistiki  katika nyanja za reli, barabara, bahari na anga, na kufika kwenye soko la umoja huo lenye watu milioni 180, pia ni miongoni mwa mada zilizopatiwa kipaumbele katika mkutano huo. 

Kwa kuzingatia nafasi muhimu ya Shirika la Reli la Iran katika kuunganisha njia za usafiri za kieneo, mkutano huu pia ni fursa nzuri ya kutambulisha uwezo na miradi ya maendeleo ya mtandao wa reli ya nchi, kuvutia uwekezaji na ushirikiano wa pamoja katika miradi ya miundombinu, kuanzisha miungano maalumu ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi, na kubadilishana mawazo moja kwa moja na watunga sera na wanaharakati wa masuala ya uchumi wa nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.

Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia ni muungano wa kiuchumi unaojumuisha Belarus, Kazakhstan, Russia, Kyrgyzstan na Armenia. Wanachama waangalizi wa umoja huo ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uzbekistan na Cuba. Iran ilijiunga na umoja huo kama mwanachama mwangalizi mwaka 2024. 

Makubaliano ya Biashara Huria ya Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia-Iran yalianza kutekelezwa tarehe 15 Mei 2025, na hivyo kufungua njia ya mauzo ya nje ya Iran katika masoko ya nchi tano wanachama wa umoja huo. Mkataba huo umeondoa ushuru wa forodha kwa asilimia 87 ya bidhaa zinazouzwa na umetoa fursa nyingi za mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Ushirikiano wa kibiashara wa Iran na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia una umuhimu wa kimkakati kwa sababu unafungua njia mpya za mauzo ya nje, kupunguza utegemezi kwa sarafu za kigeni, na kuzidisha ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda. Ushirikiano huu unaweza kuifanya Iran kuwa mchezaji mkuu katika kudhamini bidhaa mbalimbali eneo la Eurasia.

Kijiografia, Iran iko kwenye makutano ya Mashariki na Magharibi na inaweza kuwa na nafasi muhimu katika usafirishaji wa bidhaa kati ya Asia na Ulaya. Wakati huo huo, kuondolewa kwa ushuru, bidhaa za kilimo, viwanda na maarifa za Iran ni fursa zaidi za kuingia katika soko la Eurasia. Maeneo kama vile usalama wa mtandao, mawasiliano, tiba na dawa na nishati pia yamejumuishwa katika ajenda ya ushirikiano kati ya Iran na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.

Maafisa wa Umoja wa Eurasia wametangaza kuwa upeo wa ushirikiano wa jumuiya hiyo na Iran unavuka makubaliano ya sasa na utajumuisha uwekezaji wa pamoja, uhamishaji wa teknolojia na ushirikiano wa kiviwanda. Kwa msingi huo, mabadiliko ya kimkakati yanayotokana na kupanuka ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia ni pamoja na kuboresha nafasi ya kiuchumi ya Iran, kuongeza mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za mafuta, kupunguza utegemezi kwa fedha za kigeni, na kuwa na nafasi katika utaratibu mpya wa kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *