Kwa mujibu wa taarifa za serikali, waliokamatwa watashtakiwa katika mahakama za kijeshi kwa tuhuma za uchochezi na kuhamasisha ghasia. Ingawa matokeo rasmi ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa Jumamosi, Oktoba 26, tayari matarajio ni kwamba Rais Paul Biya ambaye ameitawala Cameroon tangu mwaka 1982 na ni mmoja wa marais waliodumu madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani, ataibuka mshindi tena.

Polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu Yaoundé na mji wa Garoua kaskazini mwa nchi hiyo siku ya Jumanne. Waandamanaji hao walikuwa wakipinga kile wanachodai kuwa njama za Tume ya Uchaguzi kumtangaza Rais Biya mshindi wa uchaguzi uliofanyika Oktoba 12.

Sehemu ya matokeo yasiyo rasmi yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya ndani yanaonyesha kuwa Biya anaongoza kwa asilimia kubwa ya kura. Hata hivyo, mpinzani wake mkuu, Issa Tchiroma alijitangaza mshindi siku mbili baada ya uchaguzi, akidai kupitia mitandao ya kijamii kwamba amepata ushindi wa zaidi ya asilimia 80 ya kura katika vituo mbalimbali vya kupigia kura

Cameroon Yaoundé 2025 | Wapiga kura wakiweka alama za vidole kabla ya kupiga kura katika uchaguzi wa urais
Mpiga kura akiweka alama ya kidole gumba kwenye hati kabla ya kupiga kura katika kituo cha kupigia kura wakati wa uchaguzi wa urais huko Yaounde, Cameroon, Oktoba 12, 2025.Picha: Kepseu/IMAGO

Maandamano yaenea kwenye miji kadhaa

Maandamano yameenea katika miji kadhaa ikiwemo Bafoussam, Dschang, Kousseri na Douala, ambako raia wanalalamikia hila katika mchakato wa uchaguzi, wakisema haukuwa wazi wala huru Wanasema hali hiyo ni kielelezo cha ufisadi na huduma duni za kijamii, licha ya utajiri mkubwa wa mafuta na rasilimali nyingine ambazo Cameroon inamiliki.

Serikali, kwa upande wake, imethibitisha kuwa watu zaidi ya 20 wamekamatwa na watashtakiwa kwa makosa ya uchochezi, uasi na kusababisha ghasia, kama alivyoeleza Waziri wa Mambo ya Ndani Paul Atanga Nji. Waziri huyo amesema kesi hizo zitashughulikiwa na mahakama za kijeshi, hatua ambayo imezua ukosoaji kutoka kwa mashirika ya haki za binadamu.

Wadadisi wa siasa wanasema ushindi wa Biya hautakuwa wa kushangaza, ikizingatiwa kuwa vyama vya upinzani vilishindwa kuungana, jambo lililompa nafasi ya wazi rais huyo mkongwe ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40.

Hata hivyo, ikiwa Biya atatangazwa mshindi kama inavyotarajiwa, anaweza kuendelea kutawala hadi kufikisha karibu miaka 100 ya umri, jambo linaloibua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa demokrasia na mabadiliko ya uongozi nchini Cameroon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *