
Polisi nchini Uganda imesema mabasi mawili na magari mengine mawili yamegongana na kusababisha ajali mapema leo Jumatano kwenye barabara kuu magharibi mwa nchi hiyo na kuua takriban watu 46 na kujeruhi wengine kadhaa.
Msemaji wa Idara ya polisi wa usalama barabarani Michael Kananura amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
”Wakati uchunguzi ukiendelea, tunawaomba sana madereva wote wa magari kuwa waangalifu sana wawapo barabarani, hasa kuepuka njia hatari na ambazo zimesalia kuwa moja ya sababu kuu za ajali nchini. Tunatoa pole kwa familia za marehemu na tunawatakia ahueni ya haraka majeruhi” amesema Kananura.
Ripoti ya hivi karibuni kuhusu ajali za barabarani nchini Uganda iliyotolewa na polisi ilisema kwamba asilimia 44.5 ya ajali zilizorekodiwa mwaka 2024 zilisababishwa na mwendokasi barabarani.
Watu 5,144 waliuawa katika ajali za barabarani mwaka uliopita, idadi hiyo ikiongezeka kutoka watu 4,806 mwaka 2023.