Polisi ya Uganda imeripoti kuwa watu 46 wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha mabasi mawili katika barabara kuu ya Kampala kuelekea Gulu nchini humo mapema leo Jumatano.

Nchi hiyo ya Afrika mashariki ina rekodi mbaya ya usalama barabarani, ambapo ajali za mabasi na malori hutokea mara kwa mara kwenye barabara kuu za nchi hiyo.  

Ajali ya karibuni kabisa ilitokea katika barabara kuu ya Kampala-Gulu wilayani Kiryandongo ikihusisha mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso. 

Awali polisi ya Uganda ilitangaza kuwa ajali ya leo imeuwa watu 63 na kisha ikarekebisha taarifa hiyo na kuripoti kuwa watu 46 ndio waliopoteza maisha katika ajali ya leo. 

Majeruhi wa ajali ya leo nchini Uganda wamepelekwa katika Hospitali ya Kiryandongo na vituo vingine vya karibu kwa ajili ya matibabu. 

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametuma salamu za pole na rambirambi kwa familia za wahanga wa ajali hiyo mbaya na kuwataka madereva kuwa makini wakiwa barabarani. 

Polisi ya Uganda imekuwa ikiwahimiza madereva kuchukua tahadhari kubwa; hata hivyo ajali za barabarani zimekuwa jambo la kawaida nchini humo. 

Ripoti ya matukio ya jinai ya mwaka  2024 imeweka wazi kuhusu ongezeko la asilimia sita la ajali mbaya kutoka mwaka uliopita, ikionyesha ajali mbaya za barabarani 4,434 zilizosababisha kupoteza maisha watu 5,144 nchini Uganda.

Mwaka jana pekee, watu 26 walipoteza maisha baada ya lori kupinduka na kuwaka moto katika barabara kuu ya Kampala- Gulu. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *