
Supastaa, Hakim Ziyech amekubali kujiunga bure na klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco baada ya kutokuwa kwenye timu yoyote kwa kipindi cha miezi mitano.
Mkali huyo wa zamani wa Chelsea, ambaye amekuwa akiichezea Morocco kwenye soka la kimataifa baada ya kuachana na Uholanzi alikozaliwa na ambako alizichezea timu za vijana chini ya umri wa miaka 20 na 21.
Kiungo Ziyech alitua Stamford Bridge katika msimu wa 2020/21 akitokea kwenye kikosi cha Ajax ya Uholanzi kwa ada ya uhamisho ya Pauni 40 milioni (Sh133 bilioni)
Katika misimu yake miwili ya kwanza kwenye kikosi cha Chelsea alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu la FIFA. Alipokuwa Ajax, alifanikiwa pia kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu wa 2018-19.
Kwenye kikosi cha Chelsea alicheza mechi 107 kati ya 2020 hadi 2023, alihusika kwenye mabao 27, akifunga 14 na kuasisti 13.
Ziyech, ambaye alipachikwa jina la “mchawi” kutokana na mavitu yake matata ndani ya uwanja, ameshuka kiwango chake kipindi cha karibuni, ambapo msimu uliopita alijiunga Galatasaray ya Uturuki, ambayo ilimtumia hadi Januari 2025 ilipositisha mkataba wake kwa makubaliano ya pande mbili baada ya kuichezea timu hiyo katika mechi 23.
Baada ya hapo, Ziyech alitimkia Qatar kujiunga na Al-Duhail. Kwenye kikosi hicho alicheza mechi tisa na kufunga bao moja kabla ya mkataba wake kusitishwa baada ya miezi minne tu.
Ziyech, 32, alikuwa huru kwa miezi mitano akiwa hana timu yoyote ya kuichezea na klabu kadhaa ikiwamo Bologna na Fiorentina za Italia zilihitaji saini yake. Sevilla ya Hispania nayo ilimhitaji.
CFJ 1907 Cluj ya Romania nayo ilimtaka na ilionekana angekwenda kujiunga na timu hiyo. Hata hivyo, dili hilo lilishindwa kukamilika kwa sababu Ziyech alikuwa akihitaji mshahara mkubwa.
Mmiliki wa klabu hiyo ya Romania, tajiri Ioan Varga amesema: “Ziyech amefeli, anatatizo kwenye goti lake la kushoto hicho ndicho nilichoelezwa. Ni mchezaji mzuri, lakini siwezi kupoteza pesa nyingi kwa mchezaji mgonjwa. Nilimtazama pia kwenye mechi za Galatasaray, alikuwa akicheza kwa woga. Tuliamua kujitoa kwenye mazungumzo. Alitaka mshahara wa Euro 2.5 milioni ambayo ni takribani na bilioni saba na milioni 226 kwa mwaka. Sikuwa tayari kutoa pesa hizo kwa mchezaji ambaye huna uhakika wa kumtumia.”
Kwanini Wydad?
Kuna sababu nyingi zimechangia Ziyech kufanya uamuzi wa kujiunga na Wydad. Mabosi wakubwa wa soka la Morocco wameripotiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kumshawishi Ziyech kwenda kucheza soka lake kwenye moja ya timu za nchi hiyo. Na kwenye hilo, Wydad iliweka mezani mradi wao mzuri wa kimichezo ambao ulimvutia kiungo huyo. Lakini, kubwa kabisa Ziyech alitaka kurudi kucheza soka kwenye nchi yake ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kulipaisha zaidi soka la nchi hiyo.
Mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona uzoefu wa Ziyech na ufundi wake utakavyoweza kukisaidia kikosi cha Wydad, chenye mastaa wengine kibao akiwamo Stephane Aziz Ki kinafikia malengo makubwa. Wydad inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ya Morocco, Botola Pro League, ikiwa nyuma kwa pointi moja tu dhidi ya vinara Maghreb of Fez, lakini bado ina mchezo mmoja mkononi.
Atakavyocheza na Aziz Ki
Staili ya uchezaji ya Ziyech ni ya kipekee. Ziyech anapenda kucheza kwenye wingi ya kulia na anapenda kupokea mipira akiwa pembeni sana, kisha anaingia na mpira kati, huku silaha yake kubwa ikiwa ni mguu wake wa kushoto ambao umekuwa tishio kwa makipa wengi kwa kupiga mashuti, pasi za kupenyeza au krosi.
Aziz Ki, ambaye alijiunga na Wydad akitokea Yanga ya Tanzania naye ni hodari kwa kutumia mguu wa kushoto, lakini tofauti yake amekuwa akipenda kucheza kwenye eneo la Namba 10. Ziyech naye, amekuwa akipenda kuingia kwenye eneo hilo, hivyo kitu ambacho kitafanyika watakuwa wakipishana kwenye eneo hilo, huku wote wakiwa ni hatari kwa pasi za mwisho kwa wachezaji wenzao na ubora wa kupiga mashuti kuelekea golini hasa wanaposhambulia kutokea kwenye upande wa kulia.
Ziyech amekuwa na utulivu mkubwa anapokuwa na mpira kwenye miguu yake, kitu ambacho Aziz Ki amekuwa akikifanya pia, hivyo uwepo wa mastaa hao wawili kucheza kwenye kikosi kimoja kitamfanya washambuliaji wa kati wa Wydad kuwa bize kwenye kutumbukiza mipira nyavuni kutokana na kucheza mbele ya mastaa hao wawili kiboko kwa kupiga pasi za mwisho.
Ziyech anapiga mashuti ya mbali na Aziz Ki anapiga pia, hivyo Wydad itakuwa na faida moja ya kuwa na wachezaji wawili ambao wanaweza kutengeneza matokeo wakiwa kwenye eneo lolote lile karibu na goli la wapinzani. Ni suala la kusubiri na kuona jinsi Ziyech na Aziz Ki watakavyokuwa wakipika mambo yao kwenye kikosi cha Wydad msimu huu.