Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1447 Hijria mwafaka na tarehe 23 Oktoba 2025 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 236 iliyopita yaani tarehe Mosi Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1211, alifariki dunia mshairi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Kadhim Tamimi Baghdadi, maarufu kwa jina la Uzri akiwa na umri wa miaka 80.
Alikuwa msomi na mwanafasihi mkubwa na ameacha diwani ya mashairi. Miongoni mwa mashairi ya malenga huyu maarufu wa Kiislamu ni shairi maarufu la “Al Uzriya” ambalo linamsifu Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kizazi chake kitukufu na kubainisha misingi ya dini ya Uislamu. Shairi hilo lina zaidi ya beti 1000.

Miaka 153 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Theophile Gautier, malenga na mwandishi wa Kifaransa. Gautier alizaliwa mwaka 1811 na kuhitimu masomo yake huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa.
Theophile Gautier kwa muda fulani alikuwa mwandishi wa gazeti na alikuwa na hamu kubwa ya kuwa mchoraji au mwanamuziki. Lakini hatimaye alijifunza fasihi hususan mashairi na kuacha athari maarufu katika uwanja huo.

Katika siku kama ya leo miaka 138 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Ayatullah Mirza Muhammad Hassan Husseini Shirazi alitoa fatuwa maarufu ya kuharamisha tumbaku ili kuzuia uporaji uliokuwa ukifanywa na wakoloni wa Kiingereza katika nchi za Kiislamu.
Fatuwa hiyo ilitolewa baada ya mfalme Nasiruddin Shah wa Iran kutia saini mkataba wa kuipa kampuni moja ya utawala wa kikoloni wa Uingereza mamlaka ya kuuza na kununua tumbaku ya Iran kwa kipindi cha miaka 50. Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa hiyo ya kuharamisha tumbaku.
Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, vita vya kihistoria vilivyopewa jina la al-Alamein vilitokea katika mji wenye jina kama hilo huko kaskazini mwa Misri kati ya wanajeshi wa Uingereza na jeshi la Manazi wa Ujerumani.
Vita hivyo vilimalizika baada ya kushindwa jeshi la Ujerumani, japokuwa mapigano kati ya pande hizo mbili yaliendelea katika maeneo mengine ya kaskazini mwa Afrika.
Amani kamili ilipatikana katika maeneo hayo baada ya kushindwa kikamilifu jeshi la Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. *

Na miaka 48 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama iliyotekelezwa na askari usalama wa utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, nchini Iraq.
Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria Shamsia katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa ajili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27.
Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake, Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.
