Asasi za kijamii zakemea kejeli dhidi ya wagombea wanawakeAsasi za kijamii zakemea kejeli dhidi ya wagombea wanawake

Wakazi wa Tanzania wanaendelea kuelezea matarajio yao kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, ambapo rais mpya na serikali mpya watachaguliwa. Miongoni mwao ni Esther Kasanga, mkazi wa Dar es Salaam, ambaye ana matumaini makubwa kuhusu hatima ya taifa. “Kwa kiongozi atakayechaguliwa, naomba awe kipaumbele cha mahitaji ya wananchi, hasa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu,” alisema Kasanga akizungumza na DW.

Tanzania imeendelea kutawaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, mtaalamu wa siasa Paternus Niyegira anaeleza kuwa kuna makundi matatu makuu ya wapiga kura: wafuasi wa chama tawala, wanaoamini mfumo ni thabiti; wafuasi wa upinzani, wanaodai ukosefu wa uwazi; na kundi jipya la vijana wa mitandaoni linaloonyesha hasira na kutaka maandamano siku ya uchaguzi. “Hili kundi la tatu limekuwa likiongeza msukumo wa mvutano wa kisiasa nchini,” alisema Niyegira.

Kwa Caro Mwisraeli, mwanafunzi wa uuguzi mwenye mtoto mmoja, sekta ya afya inahitaji mageuzi makubwa, hasa katika huduma za afya ya mama na mtoto. “Wanawake bado wanapata changamoto nyingi kupata huduma bora. Serikali imejitahidi, lakini vituo vya afya vinapaswa kujengwa karibu zaidi na jamii,” alisema. Kulingana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania imepunguza vifo vya akina mama wajawazito kutoka 556 kwa kila vizazi 100,000 mwaka 2016 hadi 238 mwaka 2023, lakini maeneo ya vijijini bado yana changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma.

Uchaguzi Mkuu Tanzania 2025
Wananchi wakikagua majina yao kwenye orodha ya kudumu ya wapigakura. Tanzania itafanya uchaguzi wake mkuu Oktoba 29, 2025Picha: Eric Amos/DW

Afya bora, elimu imara na ajira kwa vijana yapewa kipaumbele na wapiga kura

Wengine kama Asha Mwinuka, mkazi wa Morogoro, wanasema wanatarajia serikali mpya iweke kipaumbele katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. “Mara nyingi wagonjwa wanalazimika kununua dawa nje ya hospitali, jambo linaloongeza gharama kwa familia maskini,” alisema. Kwa upande wake, Salum Kimario wa Tanga anasema, “Huduma za afya zinahitaji usimamizi wa karibu, hasa vijijini, ambako madaktari ni wachache.”

Elimu pia ni miongoni mwa maeneo yenye matarajio makubwa. David Ndunguru, mwalimu wa shule ya sekondari jijini Mwanza, anasema: “Tunataka rais ajaye afanye mageuzi makubwa kwenye elimu. Mtaala uendane na soko la ajira la sasa duniani.” Ripoti ya UNESCO 2024 inaonyesha kuwa ingawa idadi ya wanafunzi wanaomaliza shule imeongezeka, changamoto zipo katika ubora wa elimu, ukosefu wa vifaa vya kujifunzia, na maslahi duni ya walimu.

Rehema Luhanga, mzazi kutoka Iringa, anaongeza kuwa wazazi wanatarajia mabadiliko yatakayowezesha elimu bora zaidi kwa watoto. “Watoto wetu wanahitaji siyo tu elimu ya darasani bali pia maarifa ya vitendo,” alisema. Wanafunzi kadhaa waliohojiwa walisema wanatumaini serikali ijayo itawekeza zaidi kwenye teknolojia shuleni na kupunguza ukosefu wa walimu katika maeneo ya vijijini.

Uchaguzi Tanzania 2025: Watanzania Wanataka Nini Kibadilike?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Vijana nao wana matumaini ya kuona sera madhubuti za kuwawezesha kiuchumi. Daniel Mushi, kijana mfanyabiashara mdogo kutoka Mbeya, anasema: “Natarajia rais mpya atajikita kwenye ajira kwa vijana na kuwawezesha kupitia mikopo midogo.” Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana nchini kimebaki karibu 11%, huku vijana wengi wakitegemea biashara ndogondogo zisizo rasmi. Serikali imeanzisha miradi kama TAJETI na Youth Fund, lakini changamoto za upatikanaji wa mtaji bado ni kubwa.

Mchumi Dkt. Bravious Kahyoza anasema kuwa hali ya uchumi na siasa nchini ni tulivu, ingawa matarajio ya wananchi ni makubwa. “Uchumi unategemea imani ya wananchi. Kwa sasa ishara zinaonyesha uthabiti — ukuaji uko juu ya asilimia 5, na mfumuko wa bei uko chini ya asilimia 4,” alisema. Serikali imeahidi kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, huku jeshi likihakikishia usalama wa taifa. Hata hivyo, baadhi ya wananchi bado wana wasiwasi kuhusu siku ya uchaguzi, wakitarajia serikali ijayo italeta matumaini mapya na mageuzi yanayogusa maisha yao ya kila siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *