HISTORIA mpya itaandikwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam, wakati matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC itakapocheza dhidi ya Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo, Mabaharia wa KMKM kutokea visiwani Zanzibar.
Mechi hiyo itakayopigwa saa 11:00 jioni, ni ya raundi ya pili Kombe la Shirikisho Afrika na Azam inaingia ikihitaji ushindi au sare ya aina yoyote, baada ya pambano la kwanza lililopigwa Zanzibar kushinda mabao 2-0, Oktoba 18, 2025.
Katika mechi hiyo ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, mabao ya Azam yalifungwa na mshambuliaji, Jephte Kitambala Bola dakika ya 6 na beki wa kushoto, Pascal Msindo dakika ya 42.

Wakati Azam ikihitaji sare au ushindi wa aina yoyote, kwa upande wa KMKM inahitaji kushinda angalau kwa tofauti ya mabao 3-0, ili itinge hatua ya makundi, kwani kabla ya hapo timu hizo zote mbili hazijawahi kucheza makundi katika michuano ya CAF tangu zimeasisiwa.
Rekodi kubwa ya Azam katika michuano ya CAF ni kutolewa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2013 na FAR Rabat ya Morocco kwa mabao 2-1, iliyofungwa ugenini, baada ya mechi ya kwanza Dar es Salaam kulazimishwa suluhu (0-0).

Katika raundi ya awali, Azam ilipata ushindi wa mabao 8-1 dhidi ya El Nasir ya Sudan Kusini, kisha kuitoa Barrack Young Controller II ya Liberia kwa mabao 2-1, japo safari hii kuna uwezekano mkubwa ikaandika historia mpya tangu kuanzishwa.
Kwa upande wa KMKM iliyorejea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza kwa msimu huu baada ya miaka 14, tangu iliposhiriki mwaka 2011, licha ya mafanikio makubwa Zanzibar, ila haina rekodi nzuri hata kwenye Ligi ya Mabingwa.
KMKM inayoongoza kwa mataji tisa ya Ligi Kuu ya Zanzibar, ikitwaa mwaka 1984, 1986, 2004, 2013, 2014, 2019, 2021, 2022 na 2023, imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia 2005, 2014, 2015, 2020 na 2022 na mara zote imeshindwa pia kutamba.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kassim Liogope, amesema licha ya presha kubwa nje ya uwanja lakini wachezaji wanatakiwa kusahau matokeo ya kwanza, kwa sababu kama waliweza kushinda ugenini hata wapinzani wao wanaweza kufanya kile walichofanya pia.
“Tunahitaji kucheza kama tumepoteza mechi ya kwanza, hii itatusaidia kuhakikisha tunatengeneza balansi na kuondoa ile presha iliyopo ya kuamini tumemaliza kazi, tulichokifanya ugenini kimetupa morali ya kupambana zaidi,” amesema Liogope.

Kwa upande wa Kocha wa KMKM, Hababuu Ali, amesema licha ya kuruhusu idadi kubwa ya mabao lakini bado wana nafasi ya kufanya vizuri, ingawa wanahitaji kucheza kwa tahadhari, kwa maana ya kujilinda wasiruhusu bao na wakati huohuo wanashambulia.