Benki ya CRDB imewataka wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kuendelea kukumbatia matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kiuchumi na kufikia maendeleo ya haraka.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Wateja wa Awali na wa Kati wa Benki hiyo, Bonaventura Paul wakati wa uzinduzi wa kampeni ya “Tushavuka Huko” baada ya maboresho ya mifumo ya uendeshaji wa benki hiyo.

Kwa mujibu wa Bonaventura, matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali yamekuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Tunatambua kuwa teknolojia ndiyo injini ya maendeleo ya kisasa. Ndiyo maana tumewekeza nguvu kubwa kuhakikisha mifumo yetu inakuwa imara, salama na rafiki kwa kila mteja, kuanzia mkulima, mfanyabiashara hadi taasisi kubwa,” aliongeza.

Bonaventura amesema benki hiyo inaendelea kuwekeza katika ubunifu wa huduma za kidijitali kama Simbanking na kadi za benki ili kuwapa wateja uhuru wa kufanya miamala popote na wakati wowote bila kutegemea matawi.

“Tunataka kuona Watanzania wanapunguza utegemezi wa fedha taslimu na kutumia mifumo ya kidijitali inayowapa urahisi wa kufanya biashara zao kwa ufanisi zaidi. Huu ndio mwelekeo wa dunia na sisi kama benki tunasema, tushavuka huko,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa benki hiyo, Joseline Kamuhanda, amesema kila mteja atakayefungua akaunti mpya katika kipindi cha kampeni atapata bima ya Afya Salama yenye thamani ya shilingi 200,000 pamoja na bima ya maisha (Kava Assurance) yenye thamani ya shilingi milioni mbili.

✍ @claud_jm
#AzamTVUpdates

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *