Umoja wa Ulaya (EU) unatafuta njia ya kufadhili ulinzi na ujenzi upya wa Ukraine katika miaka ya 2026 na 2027 kwa kutumia mali za Benki Kuu ya Urusi zilizozuwiliwa katika nchi za Magharibi tangu uvamizi wa Moscow nchini Ukraine. Mali hizi, zenye thamani ya mabilioni ya euro, haziwezi kutaifishwa moja kwa moja kwa mujibu wa sheria za kimataifa, lakini EU imebuni njia ya kuzitumia bila kuvunja sheria hizo.
Tume ya Ulaya imependekeza mpango utakaowezesha serikali za Umoja wa Ulaya kutumia hadi euro bilioni 185 (takribani dola bilioni 217) kati ya euro bilioni 210 za mali za Urusi zilizozuwiliwa barani Ulaya. Hii itafanyika bila kuzinyang’anya rasmi, bali kwa kuzitumia kama dhamana ya kifedha kufadhili Ukraine.
Mwanzoni mwa vita, kampuni ya Euroclear ya Ubelgiji ilikuwa ikishikilia hati fungani za Benki Kuu ya Urusi. Hati hizo zilipokomaa, fedha zilizotokana nazo zikabaki zimekwama kutokana na vikwazo vya EU. Mpango mpya unapendekeza Euroclear iwekeze fedha hizo katika hati fungani zisizo na riba (zero-coupon bonds) zitakazotolewa na Tume ya Ulaya.
Fedha zitakazopatikana kupitia uwekezaji huo zitatumika kama “Mkopo wa Fidia” kwa Ukraine, unaotolewa kwa awamu kulingana na mahitaji. Ukraine italipa mkopo huo tu baada ya kupata fidia rasmi kutoka Urusi mara vita vitakapomalizika, ikiruhusu Kyiv kutumia fedha sasa bila kusubiri makubaliano ya amani.
Maelewano bado miongoni mwa wanachana
Kwa sasa, zaidi ya dola bilioni 300 za mali za serikali ya Urusi zimegandishwa duniani kote, huku euro bilioni 210 zikiwa barani Ulaya. Kati ya hizo, euro bilioni 185 zipo Euroclear, na euro bilioni 176 tayari zimegeuzwa kuwa fedha taslimu. Tume inakadiria kuwa euro bilioni 140 zinaweza kupatikana mara moja, baada ya kulipia mkopo wa G7 wa awali kwa Ukraine.
Mpango huu unalenga kuhakikisha Urusi inaendelea kuwa mmiliki wa fedha hizo, lakini EU itakuwa imewekeza kiwango sawa katika hati fungani zake zenye dhamana ya juu. Kwa maneno mengine, fedha hazitanyang’anywa bali zitazungushwa ili kusaidia Ukraine kwa muda mfupi.
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema hatari ya kifedha itagawanywa kati ya wanachama wote wa EU. Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Bart de Wever, amesisitiza kuwa nchi yake haitakubali mpango huo bila msingi wa kisheria madhubuti na uwiano sawa wa kugawana hatari.
Mataifa mengine kama Canada na Uingereza yameonyesha nia ya kushiriki, ingawa Marekani na Japan bado hazijajitokeza wazi. Moscow imelaani vikali pendekezo hilo, ikilitaja kama “wizi wa mali za taifa” na ikiahidi kuchukua hatua za kulipiza kisasi endapo mali zake zitachukuliwa au kutumika kinyume cha sheria.
Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya unasema umeandaa taratibu mpya za kuhakikisha mali hizo hazitafunguliwa kwa bahati mbaya bila makubaliano ya pamoja kila baada ya miezi sita, ili kuzuia upinzani wa nchi kama Hungary kuathiri mchakato huo.