Mkutano huu unajiri kabla ya mazungumzo ya kimataifa kuhusu hali ya hewa yatakayofanyika mwezi ujao, licha ya upinzani unaoongezeka kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama kuhusu hatua za kuchukua kuhusu nishati safi kwa mazingira.
Umoja wa Ulaya unapanga kupitisha lengo jipya la kupunguza kwa asilimia 90 utoaji wa gesi chafu ifikapo mwaka 2040, ili kuhakikisha kuwa bara hilo liko kwenye njia sahihi kufikia kutokuwa na utoaji wowote wa gesi chafu mwaka 2050 — hatua ambayo wanasayansi wanaitaja kuwa muhimu ili kuzuia athari mbaya zaidi za ongezeko la joto duniani.
Lengo la mwaka 2040 linakusudiwa kuwa daraja kati ya ahadi ya sasa ya kisheria ya kupunguza utoaji wa gesi chafu kwa asilimia 55 kufikia mwaka 2030 na lengo la mwaka 2050. Hata hivyo, pendekezo hili limekumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya serikali za nchi wanachama kuhusu jinsi ya kugharamia mabadiliko kuelekea matumizi ya nishati safi, huku zikikabiliana pia na changamoto za ulinzi dhidi ya uchokozi wa Urusi na kufufua uchumi wa biashara.
Licha ya kuongezeka kwa majanga ya hali ya hewa duniani, juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zimepungua kasi — hasa kutokana na hatua za Rais wa Marekani, Donald Trump za kubatilisha sera za Marekani za kupunguza utoaji wa gesi chafu na kuhimiza matumizi ya nishati mbadala.
Malengo na ushindani uliopo
Mazungumzo ya viongozi wa Umoja Ulaya yatazingatia kile kinachoitwa “masharti ya kuwezesha” — ikiwemo ufadhili na sera za kusaidia — ambazo zinahitajika ili kuepuka ongezeko la gharama za nishati kwa raia na kusaidia biashara zinazokabiliana na ushindani kutoka bidhaa za bei nafuu za China na ushuru wa Marekani.
Waziri Mkuu wa Uholanzi, Dick Schoof, amesema anatarajia Umoja wa Ulaya utaendelea kushikilia malengo yake ya mwaka 2030, ambayo takwimu rasmi zinaonyesha yanaelekea kutimizwa.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen, amewaambia viongozi kuwa mabadiliko kuelekea uchumi safi ni fursa kubwa kwa Ulaya kufufua viwanda vyake na kupunguza utegemezi kwa bidhaa kutoka China, ambayo inawekeza kwa kasi katika nishati mbadala.
Von der Leyen pia aliahidi marekebisho kadhaa, yakiwemo kudhibiti bei katika soko lijalo la kaboni kwa mafuta yanayoingia kutoka masoko ya kigeni, na kuimarisha ushuru wa mpaka wa kaboni katika umoja huo.
Rasimu ya hitimisho la mkutano wa kilele wa Umoja Ulaya, iliyoonwa na shirika la habari la Reuters, inaonyesha kuwa viongozi watakubaliana kuendelea na lengo la mwaka 2040, lakini maelezo ya mwisho yataachwa kwa mawaziri kuidhinisha katika kikao cha Novemba 4, kabla ya mkutano wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa wa COP30 utakaofanyika kuanzia Novemba 6 hadi 7.
Hitimisho hilo pia litajumuisha masharti ya marekebisho yanayoonyesha wasiwasi wa baadhi ya viongozi, ikiwemo uwezekano wa kulipunguza lengo hilo baadaye ikiwa hali itabadilika.