
WIKIENDI hii klabu za Tanzania zitakuwa na kibarua cha kuhakikisha nchi inaandika historia ya kuingiza klabu nne katika mashindano ya Klabu Afrika msimu huu.
Kwa kumbukumbu tulizonazo hapa kijiweni, hakuna nchi yoyote kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati ambayo imewahi kuingiza timu nne kwa mpigo katika hatua ya makundi ya mashindano ya klabu ya CAF.
Kati ya hizo nne zinazotegemewa, tayari tuna uhakika wa mojawapo kwa vile Azam FC inakutana na klabu nyingine ya hapa nchini KMKM hivyo yoyote itakayopita hapo sisi tutafurahia maana ni Tanzania.
Hawa jamaa mechi yao inachezwa Ijumaa hii na tayari Azam ina faida ya ushindi wa mabao 2-0 ambao iliupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa kule visiwani Zanzibar.
Halafu Jumamosi, Yanga itaikaribisha Silver Strikers ya Malawi ikihitajika kushinda kwa tofauti ya mabao mawili ili isonge mbele na kwa upande mwingine Singida Black Stars itacheza na Flambeau du Centre ya Burundi.
Jumapili Simba itafunga hesabu kwa kucheza na Nsingizini Hotspurs ya Zimbabwe halafu baada ya hapo tutajua kama hilo la timu nne kwenye hatua ya makundi limewezekana au halijawezekana.
Kwa matokeo ya mechi za mwanzo, wadau katika kijiwe chetu tuna imani kubwa kwamba Tanzania safari hii itaingiza klabu nne katika mashindano ya Klabu Afrika na hatuhitaji kuona kuna inayokwama kufanya hivyo.
Hakuna mlima mrefu wa kupanda ambao kila timu kati ya hizo inao hivyo tunategemea kuona zinatumia vizuri viwanja vya nyumbani kupata matokeo yanayohitajika ziweze kuingia katika hatua ya makundi.
Itakuwa ni aibu kwa klabu zetu kushindwa kutumia faida ya kucheza nyumbani kwenye mechi hizo.