WAKATI huu ukiwa ni msimu wa 14 kwa wekundu wa Msimbazi, Simba kucheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, meneja Dimitar Pantev pamoja na benchi lake la ufundi, watakuwa na kazi moja tu Jumapili Oktoba 26, 2025 kuifanya timu hiyo kuingia anga za Espérance, Al Ahly na Mamelodi Sundowns.

Kivipi? Al Ahly ya Misri ambao ni mabingwa wa kihistoria, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na Espérance ni miongoni mwa klabu chache ambazo zimekuwa na uhakika wa kucheza hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa miaka saba iliyopita. Kila mwaka wao wapo hatua ya makundi.

Licha ya kutokuwa na historia ya kutwaa taji katika michuano hiyo, Ligi ya Mabingwa Afrika na hata Kombe la Shirikisho, Simba inaonekana kuwa na rekodi nzuri kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kwa kujaribu kuingia anga za vigogo hao ambao wamekuwa wakitawala soka la Afrika.

Ndani ya miaka saba iliyopita, Simba imetinga hatua ya makundi ya michuano ya CAF mara sita, huku tano kati ya hizo ikiwa mfululizo, kama Pantev pamoja na msaidizi wake, Seleman Matola watafanikisha kumalizia kazi iliyosalia dhidi ya Nsingizini Hotspurs baada ya mechi ya kwanza kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, itakuwa Simba imefuzu mara sita mfululizo makundi.

Hii ni rekodi kwa timu za ukanda wa Afrika Mashariki katika awamu tano mfululizo, mara tatu ni upande wa Ligi ya Mabingwa ilikuwa msimu wa 2020–21, 2022–23 na 2023–24 na nyingine ni Shirikisho 2021–22 na msimu uliopita 2024-25 na Simba ilifika hadi fainali ikicheza dhidi ya RS Berkane.

Kwa upande wa Afrika Mashariki na Kati, ni Simba na Al Hilal Omdurman ya Sudan ambazo zimekuwa na uhakika huo, ndani ya miaka sita iliyopita imetinga hatua ya makundi.

Mbali na kutinga mara tano mfululizo hatua ya makundi kwa Simba, awamu nne walikuwa wakiishia hatua ya robo fainali, ya mwisho walimaliza jinamizi hilo kwa kufika fainali ambayo walipoteza mbele ya Berkane kwa jumla ya mabao 3-1.

Jambo kubwa zaidi, Pantev ana mtihani wa kuivusha Simba kucheza makundi, kisha kuitoa hapo kwenda robo fainali kama ilivyozoeleka, lakini kuipeleka mbali zaidi mtihani alioufuzu Fadlu Davids msimu uliopita. Nyongeza, kubeba kombe ndio rekodi inayosubiriwa zaidi Simba.

Miongoni mwa makocha ambao wamepita Simba na wana historia nzuri katika michuano hiyo ya kimataifa, Patrick Aussems ameitaja timu hiyo haipo mbali kutwaa ubingwa wa Afrika kutokana na muendelezo wake.

“Muendelezo ndiyo kitu muhimu, Simba hawapo mbali, niwe mkweli, siku zote hicho ndicho kitu muhimu, inahitaji kujaribu mara kwa mara kabla ya kufanikiwa, tulipambana wakati wangu na kufika robo, ilikuwa ni hatua nzuri,” amesema na kuongeza;

“Wakati nikiwa Tanzania naifundisha Singida Black Stars, niliona wanakikosi kizuri kwa hiyo nategemea kuona wakiendelea kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF na ili ufanikiwe unatakiwa kuwa tayari kukabiliana na timu za Kaskazini na Mgharibi mwa Afrika.”

Aussems alikuwa kocha wa Simba mwaka 2018 na aliiongoza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ilitolewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1 katika mechi mbili.

Baada ya mafanikio hayo, Aussems alisaini mkataba mpya wa mwaka mmoja kuendelea kuwa kocha mkuu wa timu hiyo kwa msimu wa 2019/20. Hata hivyo, Novemba 2019, uongozi wa Simba uliachana naye kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Sasa ni miaka saba baadae na kikosi hicho kipo chini ya Pantev ambaye ana kibarua cha kuendeleza historia hiyo.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi hicho, kocha huyo amesema yanaendelea vizuri na anaamini mashabiki wa timu hiyo watafurahia soka safi wikiendi ijayo.

“Hatutakiwi kuona tayari tumefika hatua ya makundi, tunatakiwa kusahau matokeo ya mechi ya kwanza, ile ilikuwa ni nusu ya safari, tunatakiwa kumaliza kazi kwa kufanya vizuri pia kwenye mechi ya marudiano,” amesema kocha huyo na kuongeza;

“Tumekuwa na mazoezi tofauti yaliyolenga kuboresha kiwango chetu ili tuwe kwenye ubora ambao utatufanya kutimiza kile ambacho tunahitaji.”

UKUBWA AFRIKA

Wakati Simba ikiwa na robo fainali tano na fainali moja ya CAF kwa misimu sita iliyopita, Mamelodi Sundowns yenyewe ina robo tatu, nusu mbili na fainali moja ambayo ilicheza msimu uliopita na kufungwa dhidi ya Pyramids anayoichezea mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele kwa jumla ya mabao 3-2.

Upande mwingine, Al Ahly yenyewe imebeba mara nne kwenye msimu wa 2019–20, 2020–21, 2022–23 na 2023–24. Msimu wa 2021-22 walipoteza fainali dhidi ya Wydad Casablanca kwa mabao 2-0 huku msimu uliopita walitolewa katika hatua ya nusu fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns kwa kanuni ya bao la ugenini.

Katika mechi ya kwanza, Mamelodi Sundowns ikiwa nyumbani walitoa suluhu (0-0) walipoenda Cairo wakatoka sare ya bao 1-1. Kwa upande wa Espérance Sportive de Tunis ya Tunisia ina robo fainali tatu, nusu mbili na fainali moja ambayo ilipoteza mwaka jana, 2024 mbele ya Al Ahly.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *