Marekani. Ikulu nchini Marekani imekanusha tetesi zinazodai Rais Donald Trump, anapanga kumpunguzia adhabu nguli wa hiphop, Sean “Diddy” Combs.
Kupitia taarifa rasmi ya maafisa wa Ikulu imeweka wazi kuwa hakuna mpango wowote wa kumfutia wala kumpunguzia adhabu Diddy. Na kwamba taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari ni za uongo.
“Hakuna ukweli hata kidogo katika ripoti hiyo ya kumuachia au kumpunguzia adhabu Combs,” walisema maafisa hao.

Utakumbuka vyombo mbalimbali vya habari Marekani viliripoti kuwa Trump anampango wa kumfutia kesi Diddy ambaye anakabiliwa na mashitaka mazito ya usafirishaji wa binadamu kwa ajili ya biashara za kingono.
Hata hivyo, kwa mujibu wa wasemaji wa Ikulu wanaeleza kuwa suala hilo halijawahi kujadiliwa kabisa katika ofisi ya Rais.
Nguli huyo wa muziki wa hip hop, Sean “Diddy” Combs, alikamatwa kwa mara ya kwanza Septemba 16, 2024 jijini New York baada ya kufunguliwa kesi mahakamani na zaidi ya watu 10 akiwemo aliyekuwa mpenzi wake Cassie.
Aidha Oktoba 3,2025, mahakama ilimhukumu kifungo cha miezi 50 sawa na miaka 4 na miezi 2 katika gereza la shirikisho la Metropolitan Detention Center, lililopo Brooklyn, New York.
Diddy amewahi kutamba na ngoma kama I’ll Be Missing You, Last Night, Coming Home iliyopenya kwenye chati za Billboard, Bad Boy for Life, I Need a Girl (Part 1 & 2) na nyinginezo.