
Chanzo cha picha, Facebook/Heche
Ndugu wa makamu mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania CHADEMA Edward Heche amesema kwamba Ndugu yake John Heche hajulikani alipo baada ya kuwasiliana na maafisa wa polisi.
Akizungumza na BBC , Edward Heche ambaye pia ni ndugu mdogo wa John Heche amesema kwamba maafisa wa polisi wamemwambia hawana taarifa zozote kuhusu kuzuiliwa kwa ndugu yake na kwamba hakuna mashtaka yoyote yaliopangwa dhidi yake.
‘Nimewasiliana na Polisi wa Tarime kuthibitisha iwapo ameletwa hapa ili kufunguliwa mashtaka, lakini tumeambiwa kwamba hajafikishwa, hakuna ripoti rasmi kwamba atafikishwa Tarime’ na kwamba hawatarjii kwamba ataletwa eneo hilo’, alisema.
Siku ya Jumatano, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilisema kuwa John Heche, alikuwa amesafirishwa hadi Tarime na Jeshi la Polisi baada ya kukamatwa mapema siku hiyo.
Gaston Garubindi, wakili mkurugenzi wa Sheria CHADEMA, alithibitisha hilo na kusema “Mheshimiwa Heche alikamatwa na jeshi la Polisi alipokuwa mahakamani kwa makosa ambayo hawajasema.
Lakini akizungumza na Mdogo wake huyo amesema kwamba aliwasiliana na afande Muliro wa Dar es Salaam ambaye alisema kwamba hawamzuilii kiongozi huyo na kwamba hawana madai yoyote ya kesi dhidi yake.
Alisema kwamba vilevile amewasiliana na mkuu wa kitaifa kuhusu uhamiaji ambaye alimthibitishia kwamba idara yake Haimzuilii Bwana heche na kwamba haina kesi yoyote kuhusu kiongozi huyo.
Edward ameongeza kuwa kwamba licha ya kuwa hakuna ripoti zozote kuhusu aliko kiongozi huyo, hajapewa haki zake za kuonana na wanafamilia au wakili wake.
”Hatujui iwapo yuko salama au la hatujui anakula nini’, yote haya ni kinyume na katiba’, alisema bwana Edward.
Amesema kwamba amewasiliana na uongozi wa Chadema kuhusu hatua za kuchukua .
Heche alikamatwa mwishoni mwa juma lililopita mkoani Mara kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya huko Isibania One Stop Border alipokuwa anataka kuingia Kenya.
Kwa mujibu wa CHADEMA, Heche alikuwa akiingia nchini Kenya kukiwakilisha chama kwenye shughuli za mazishi ya mwanasiasa nguli wa Kenya,Raila Amolo Odinga.
Pamoja na kumuweka kizuizini taarifa ya chama hicho ilisema kuwa, Mamlaka ya Uhamiaji Tanzania ilimnyang’anya hati yake ya kusafiria.
Idara ya Uhamiaji ilisema kwenye taarifa yake kuwa Heche aliondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu na kanuni za Uhamiaji.
Ilitoa wito kwa Watanzania na wageni wanaotoka na kuingia Tanzania kufuata utaratibu na kanuni zinazoongoza uingiaji, ukaazi na utokaji wa watu nchini ili kuepuka kutenda kosa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
John Mnyika amesema madai ya Idara ya Uhamiaji kuwa Heche alivuka mpaka kuingia Kenya kinyume cha utaratibu si ya kweli na kuhusisha madai hayo na kitendo cha kumkamata hii leo.
BBC Imetafuta mamlaka za polisi Tanzania lakini hawajapatikana lakini juhudi bado zinaendelea.