
Chanzo cha picha, Ruto/Facebook
Mahakama kuu nchini Kenya imesitisha kwa muda utekelezaji wa kipengele cha sheria inayohusu matumizi mabaya ya mitandaoni.
Kipengele hicho kinafafanua kosa la unyanyasaji wa mtandaoni yaani pale mtu anapotumia mtandao kumdhalilisha au kumtishia mtu mwingine.
Uamuzi huu ulitolewa na Jaji Lawrence Mugambi wa Mahakama ya milimani Jijini Nairobi , Jumatano tarehe 22 Oktoba mwaka huu. Mahakama iliamua kwamba marekebisho ya sheria hiyo isitekelezwe kwa sasa hadi pale kesi iliyowasilishwa kupinga sheria hiyo itakapozikilizwa na kuamuliwa rasmi.
Kesi hiyo iliwasilishwa na Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya pamoja na mwanaharakati na mwanamuziki Reuben Kigame, ambaye pia aliwahi kugombea urais wa Kenya. Wanasema kwamba vipengele hivyo vipya:
- Vinatoa maelezo yasiyoeleweka vizuri kuhusu nini hasa ni kosa,
- VInapunguza uhuru wa watu kujieleza mitandaoni,
- Na inaathiri sheria ya awali ya kulinda taarifa binafsi za watu (Data Protection Act ya mwaka 2019).
Lakini ilifikaje hapa hadi kwa wawili hao kwenda kutafuta haki mahakamani?
Mapema ya Jumatano ya tarehe 15 mwezi Oktoba mwaka huu kabla ya taifa kutangaziwa kifo cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kilichotokea nchini India, Rais wa Kenya, William Ruto, alitia saini miswada minane iliyokuwa imeidhinishwa na bunge la taifa na kuifanya kuwa sheria.
Miongoni mwa miswada hiyo ni sheria muhimu zinazogusa sekta za utawala, ardhi na teknolojia.
Hata hivyo, Sheria iliyozua mjadala mkali zaidi miongoni mwa vijana wa kizazi cha Genz wa Kenya mitandaoni ni sheria ya uhalifu wa mitandaoni ambayo imeibua wasiwasi kuhusu mustakabali wa uhuru wa kidijitali nchini Kenya.
Kwa mujibu, wa sheria hiyo mpya, serikali ya Kenya ingekuwa na uwezo wa kuondoa tovuti zinazodaiwa kuendeleza uhalifu, kufuta akaunti za mitandao ya kijamii na kuzima vifaa vya kidijitali vinavyoshukiwa kuendeleza shughuli haramu kama vile ponografia.
Mswada wa sheria ya matumizi mabaya ya kompyuta na uhalifu wa mtandao (Marekebisho) 2024 unahusu nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mswada huo uliochapishwa kwa mara ya kwanza na bunge la taifa la Kenya tarehe 9 Agosti 2024, ulipitishwa baada ya mashauriano na umma, kupitiwa upya na Kamati ya bunge la taifa ya Mawasiliano, Habari, na Ubunifu.
Michango ya wadau kutoka kwa viongozi wa mashirika ya kiraia na sekta ya teknolojia pia ilishirikishwa.
Sheria hiyo inapanua maana ya ”matumizi mabaya ya kompyuta” ili kujumuisha ufikiaji au urekebishaji wa mfumo wowote bila idhini, na kutambua uhalifu wa mitandaoni kama makosa yoyote yanayolenga mitandao au data kwa kutumia miundombinu ya mawasiliano ya ICT.
Sheria hiyo mpya, inapanua ufafanuzi wa serikali ya Kenya kuhusu uhalifu wa mtandaoni na kuongeza adhabu kwa makosa ya mtandaoni.
Aidha, itaipa mamlaka uwezo mpana zaidi wa:
- Kuzuia upatikanaji wa mifumo ya kidijitali,
- Kuwashurutisha kampuni za huduma kukabidhi data ya watumiaji,
- Kuamuru kuondolewa kwa maudhui yanayochukuliwa kuwa haramu au uongo na yenye msimamo mkali.
Endapo mtu atapatikana na hatia, marekebisho hayo yanaipa Mahakama mamlaka ya kuamuru kuondolewa kwa maudhui hayo kutoka kwa jukwaa au kifaa cha dijitali kama vile simu ya mkononi.
Sheria hiyo pia imeweka adhabu kali kwa watakaohusika na makosa ya mtandaoni. Miongoni mwa adhabu hizo ni
- Faini isiyozidi shilingi milioni 20 au
- Kifungo cha hadi miaka 10 au
- Adhabu zote mbili kwa pamoja kwa yeyote atakayesambaza maudhui ya kielektroniki yenye kusababisha hofu,vurugu au uharibifu wa mali.
Kifungu cha 42A cha sheria hiyo kinasema:
“Mtu yeyote atakayechukua umiliki wa kadi simu ya mtu mwingine bila idhini, kwania ya kufanya uhalifu, atakabiliwa na faini hadi shilingi laki mbili au kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja”.
Chini ya sheria hii mpya, watoa huduma za mtandao pia wanatakiwa kuhifadhi, kutoa taarifa muhimu za watumiaji pale zitakapohitajika kwa uchunguzi unaoendelea na vyombo vya usalama.
Kwa mujibu wa sheria hii, hatua zingine za kiusalama zitahusisha:
- Ujanibishaji wa data kwa miundombinu muhimu ya taarifa (CII),
- Tathmini za kila mwaka za hatari
- Kuanzishwa kwa Vituo vya Uendeshaji wa Usalama Mtandaoni.(Cybersecurity operations Centres).
Inapatana na Kanuni Muhimu za Miundombinu ya Taarifa (Ilani ya Gazeti Na. 44, Februari 2024).
Pia, sheria hiyo ilifanyia marekebisho kipengele kingine kuhusu “phishing”, yaani pale mtu anapotumia njia ya mtandao kama barua pepe au simu kuwalaghai watu wafichue taarifa zao binafsi kama namba za kadi ya benki, nywila, au kitambulisho. Adhabu ya kosa hilo ni:
Faini ya hadi shilingi 300,000, au
Kifungo cha hadi miaka 3, au
Vyote viwili.
Mswada huo ulipendekezwa na Mbunge wa Wajir Mashariki nchini Kenya, Dawood Mohammed, ambaye alieleza unalenga kukabiliana na ongezeko la uhalifu mtandaoni nchini humo.
Upande wa serikali ya Kenya
Serikali ya Rais Ruto imetetea maekebisho hayo, ikisema yanatoa mwongozi wa kisasa wa kukabiliana na vitisho vya kidijitali vinavyozidi kuongezeka kama vile
- Ulaghai wa mtandaoni
- Taarifa potofu
- Unyanyasaji wa kimtandao
- Wizi wa maelezo ya kibinafsi
- Ulaghai kupitia kadi za simu (sim-card).
wakati huo huo, Wabunge wanaoegemea serikali wamesisitiza kuwa marekebisho hayo hayaondoi uhuru wa kikatiba wala kukabidhi mamlaka ya kutunga sheria.
Marekebisho ya sheria yamekosolewa vikali

Chanzo cha picha, David Maraga/X
Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wa upinzani wameelezea wasiwasi kuwa marekebisho haya yanatoa mamlaka makubwa kwa serikali iliyoko madarakani kudhibiti mtandao na uhuru wa kujieleza, hasa kuelekea msimu wa siasa na maandamano yanayoandaliwa na vijana kupitia mitandao ya kijamii.
Aliyekuwa jaji mkuu na pia mgombea wa urais katika kinyang’anyiro cha 2027 David Maraga amemlaumu Rais Ruto akitaja kuwa kutia saini miswada hiyo yenye utata inayohujumu raia wa kawaida na kufaidi walio nacho katika jamii.
”Wakenya wenzangu wakati tulipokuwa tuking’ang’ana na simanzi kwa kumpoteza kiongozi Raila Odinga, Rais Ruto alikuwa mbioni kutia saini miswada inayodhulumu wakenya na uifanya sheria. Hii ni aibu kwa Rais kufanya hivyo” alisema Maraga alipokuwa akihutubia wanahabari jijini Nairobi.
Alitaja marekebisho ya Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Makosa ya Mtandao kuwa yanasumbua hasa, akisema yameundwa kukandamiza upinzani na kuminya uhuru wa kisiasa.
“Marekebisho hayo yanalenga kudhibiti kujieleza kisiasa. Hatujasahau kwamba mnamo Juni 2024, vijana walipopinga Mswada wa Fedha, Rais Ruto aliwataja kuwa wahalifu na magaidi.” alisema David Maraga.
Wakenya mitandaoni wanasemaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakenya wengi mitandaoni wamesema marekebisho haya mapya yanakwenda kinyume na misingi ya kidemokrasia na uhuru wa kujieleza ambayo hayati Raila Odinga amekua akitetea kwa miongo kadhaa.
Vijana wengi wameonekana wakisambaza kauli ambayo marehemu Raila Odinga aliwahi kuandikia mitandaoni tarehe 24 mwezi Oktoba mwaka 2023 na ilisomeka
”Uhuru ambao kenya inajivunia ni wa kujieleza, na tunapaswa kuulinda kwa wivu zaidi”.Aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga.
Vijana wa Gen Z Kenya wanaona vipengee hivi vipya si kama chombo cha kupambana na uhalifu wa mtandao bali kama zana ya serikali kudhibiti nafasi ya raia kwenye majukwaa ya kidijitali.
Kenya imekuwa moja ya nchi chache barani Afrika zinazojivunia uhuru mpana wa kujieleza hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Katika miezi michache, majukwaa kama ya X(zamani twitter, Facebook,na Tiktok yamekuwa nguzo ya majadiliano ya kisiasa , uhamasishaji wa maandamani ya raia, na ufuatiliaji wa uwajibikaji wa viongozi.
Vipengee vingine vyenye utata

Chanzo cha picha, Rais Ruto/ Facebook
Kando na mswada huo wa uhalifu mitandaoni kuna miswada mingine ambayo pia ilitiwa saini na Rais Ruto na kuwa sheria.
Miswada hiyo ni pamoja na:
Muswada wa Sheria ya Ubinafsishaji 2025, Muswada wa Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori (Marekebisho) wa 2023, Muswada wa Marekebisho ya Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi 2024, Muswada wa Marekebisho ya Ada ya Huduma ya Abiria wa Hewa 2025, Mswada wa Watoa Huduma za Mali Pekee 2025, Muswada wa Marekebisho ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi, 2023 na Muswada wa Sheria ya Ardhi (Marekebisho) 2024.
Marekebisho yaliyofanyiwa sheria ya Ubinafsishaji 2025 pia yameibua wasiwasi.
Awali sheria hiyo ililazimisha serikali kutaka uidhinishaji wa bunge la taifa na wizara ya fedha kabla ya kuuza taasisi za serikali zinazopata hasara lakini sasa hawatahitaji bunge kuwakagua wanapoamua kuuza mali ya serikali.
Pia muswada wa marekebisho ya tume ya kitaifa ya ardhi 2023 itaruhusu tume ya kukagua ugawaji wa ardhi wa zamani, kusimamia fidia kwa wale walioathiriwa na makadirio ya serikali na kushughulikia migogoro ya ardhi.
Itakayoathiri watalii humu nchini ni ya Muswada wa Marekebisho ya Ada ya Huduma ya Abiria wa Hewa 2025, ambayo wakenya wanaosafiri kwa ndege kuongezea shilingi sitini na watalii wasio raia wa Kenya watatakiwa kuongeza dola hamsini kila wanaposafiri. Fedha hizo zitapelekwa kwa bodi ya utalii.
Hata hivyo, mkosoaji wa serikali ambaye aliwahi kuwa jaji mkuu David Maraga pia amelaani ushiriki mdogo wa wananchi ulioambatana na kupitishwa kwa Miswada hiyo, akilishutumu Bunge kwa kupuuza mawasilisho ya wananchi na hata wizara husika za serikali.
“Marekebisho haya ni kinyume cha sheria, ni batili, na ni batili,” alisema. “Rais Ruto amepoteza uhalali wa kuendelea kutawala nchi hii.”
Kwasasa, Mahakama Jijini Nairobi imesitisha tu kipengee cha mswada wa uhalifu wa mitandaoni lakini sheria zile zingine saba zilizotajwa mwanzoni mwa makala haya zitaanza utekelezaji wake.
Kinachosubiriwa ni kuona iwapo umma utabadilisha maoni na kipengee hicho cha kudhibiti mitandao kifutwe kabisa au baadaye serikali ya Kenya iaminishe mahakama uhalali wa mchakato mzima na kianze kutekelezwa.
Marufuku ya mitandao yalivyowakasirisha vijana wa Nepal

Chanzo cha picha, Sunil Pradhan/Anadolu via Getty Images
Haya yanajiri baada ya mataifa mbalimbali ulimwenguni hasa bara la Afrika yakishuhudia kupinga serikali kutumia sheria kuminya uhuru na demokrasia.
Taifa la hivi punde ni Nepal.
Siku chache kabla ya maandamano kuanza rasmi Nepal, serikali ilitangaza marufuku kwa majukwaa mengi ya mitandao ya kijamii kwa madai ya kutotekeleza agizo la usajili.
Vijana wengi walichukulia hatua hiyo kama mbinu ya kuwakandamiza.
Aditya na marafiki zake walikusanyika kwenye maktaba moja mjini Kathmandu na kutumia majukwaa ya akili mnembo (AI) kama ChatGPT, Grok, DeepSeek na Veed kutengeneza video 50 kuhusu rushwa na “nepo kids”.
Walitumia mitandao kupanga maandamano yaliyopelekea rais wa nchi hiyo kukimbia.
Huu ni moja ya mfano ambao vijana wamekuwa wakiitumia mitandao ya kijamii kushirikiana kuleta mageuzi serikali.

Chanzo cha picha, Abu Adem Muhammed / Anadolu via Getty Image
Mustakabali wa uhuru wa kidijitali
Bila shaka, uhalifu wa wa mitandaoni ni changamoto halisi kuanzia ulaghai wa data, udukuzi wa mifumo hadi ueneaji wa tarifa potofu.Sheria bora ya kukabilianana uhalifu huo ni muhimu kwa taifa lolote. Hata hivyo, utekelezaji wake utakuwa ni wa kuchukuliwa na uzito.
Wachanganuzi wa masuala ya haki za binadamu wanasema usalama wa mitandaoni haupaswi kuchukua nafasi ya uhuru.