TIMU 16 za wanaume na 12 za wanawake zitashiriki Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL) itakayoanza Novemba 17, mwaka huu huku ikitarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ligi hiyo ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Chinangali, Dododma ndiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa na yamekuwa na ushindani mkubwa kila mwaka.
Kamishina wa ufundi na mashindano wa shirikisho la mpira wa kikapu nchini (TBF), Daniel Mbwana aliliambia Mwanaspoti kati ya timu hizo, nne zinafuzu moja kwa moja baada ya mwaka jana kufika nusu fainali.
Alizitaja timu hizo kwa wanaume ni Dar City, ABC, JKT na Kisasa Heroes, huku kwa wanawake ni Fox Divas (Mara), DB Lioness, JKT Stars.
Alisema timu hizo zitaungana na nyingine, zitakazowakilisha kanda za kitaifa ambazo ni Kanda ya Ziwa, Dar es Salaam, Nyanda za juu Kusini, Kati, Magharibi, Kaskazini na Zanzibar.

DB Troncatti imeongezwa baada ya mwaka jana kufika nusu fainali na kushika nafasi ya tatu katika Ligi ya Kikaku ya Dar es Salaam (BDL).
“Tumeiongeza DB Troncatti baada ya DB Lioness na JKT Stars kupata nafasi ya moja kwa moja ya kushiriki Ligi ya NBL mwaka huu. Sheria iliyowekwa bingwa wa mkoa ndiye atakayeshiriki Ligi ya NBL na Ligi ya Dar es Salaam ni DB Lioness huku JKT Stars ya pili na DB Troncatti ya tatu,” aliongeza Daniel.
Mwenyekiti wa DB Troncatti, Adamu Zuberi alisema baada ya kupewa nafasi hiyo wameanza kujifua kwenye Uwanja wa Donbossco Oysterbay na wachezaji wote wamefurahia na wamehaidi kufanya vizuri.

ROBO FAINALI KESHO MWANZA
LIGI ya kikapu Mkoa wa Mwanza inatarajiwa kushuhudia robo fainali yenye ushindani mkali tofauti na miaka ya nyuma.
Robo fainali hiyo itapigwa kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa Mirongo na Planet itacheza dhidi ya Mading W11, Octopus itakichapa na Kisesa, Profile uso kwa uso na Crossover na Eagles ikipepetana na Switch.
Timu hizo zilitinga hatua hiyo baada ya Profile kushika nafasi ya kwanza kwa pointi 20, ikifuatiwa na Planet pointi 20, Eagles (20), Octopus (19), Kisesa (18) Switch (18) na Madingi WII (18).
Akiongea na Mwanaspoti kwa simu kutoka Mwanza, Katibu msaidizi wa Shirikisho la Mpira wa kikapu nchini (TBF) Benson Nyasebwa alisema ushindani katika ligi hiyo umekuwa ni mkubwa tofauti na miaka iliyopita.
Alisema ushindani umetokana na uwezo mkubwa ulionyeshwa na timu zote 12, hali iliyofanya baadhi ya timu zifungane pointi na vyingine pointi chache.
MSIMAMO—WANAUME
TIMU PLD W L PTS
Profile 11 9 2 20
Planet 11 9 2 20
Eagles 11 9 2 20
Octopus 11 8 3 19
Kisesa 11 7 4 18
Swith 11 7 4 18
Mading 11 7 4 18
Crossover 11 4 7 15
Hoopers 11 3 8 14
Spiders 11 2 9 13
Mabatini 11 1 10 12
Oratoria 11 0 10 10

DAR CITY WAJANJA HAO
BAADA ya kufuzu kucheza hatua ya pili ya mashindano ya Elite 16, Dar City imefanya usajili ikilenga mashindano ya Road to BAL Divisheni ya Mashariki.
Kocha wa mchezo huo kutoka Kinondoni, Salimu Ally alisema ilichofanya City ni ujanja na zaidi haijataka wachezaji wa kujaribu bali kupiga kazi kweli pia ikizingatiwa mashindano hayo ni magumu.
“Katika mashindano ya aina hii siyo sehemu ya majaribio bali ni muda wa kufanya vitendo kwa ajili ya hatua inayofuata.
“Mchezaji anajaribiwa kwenye mechi za kirafiki na mashindano madogo, athari ya kujaribu wachezaji katika mechi za kufuzu, ni kupoteza nafasi ambayo ni hasara katika uwekezaji,” aliongeza Ally.
Nyota wa kigeni waliosajiliwa ni Solo Diabate (Ivory coast), Deng Angoko (Sudan ya Kusini), Makh Mitchell na Raphaiel Putney (Marekani).
Nyota hao walishirikiana vizuri na wachezaji wazawa Hasheem Thabeet na Amin Mkosa aliyepata nafasi ya kucheza muda mwingi.
Kabla ya kusajili wachezaji hao ilikuwa na wachezaji Sharom Ikedigwe, Clinton Best (Nigeria), Victor Mwoka (Kenya) na Jamel Marbuary (Marekani) waliowakilisha timu hiyo katika Ligi ya BDL.

27 WASHIRIKI KATIKA MAFUNZO
Makocha 27 wameshiriki katika mafunzo ya ukocha daraja la kwanza, yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Tanga na Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kamishina wa makocha wa shirikisho la mpira wa kikapu nchini (TBF) Robert Manyerere alisema mafunzo hayo yalifanyika kwa siku tano, huku makocha 19 wakiwa ni wanaume na nane wanawake.
“Mafunzo ya nadharia yalifanyika darasani kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile majadiliano na uwasilishaji,” alisema Manyerere.
Mafunzo hayo yalifungwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Tanga, ndugu Jacob Senkondo.