Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, ametangaza kuwa nchi yake inamiliki makombora 5,000 ya kutungulia ndege yaliyotengenezwa Russia ili kukabiliana na vitisho vya jeshi la Marekani na vikosi vyake vilivyotumwa katika visiwa vya Caribbean.

Katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wakuu wa kijeshi siku ya Jumatano, Maduro alisema Venezuela ina kwa uchache makombora 5,000 ya masafa mafupi yaliyotengenezwa na Russia yanayojulikana kama Igla-S yaliyotumwa katika maeneo muhimu ya ulinzi wa anga “ili kulinda amani.”

Baada ya Marekani kufanya mashambulizi kadhaa katika pwani ya Venezuela Septemba mwaka jana, ikilenga boti ilizodai kuwa zinatumika kwa ajili ya magendo ya dawa za kulevya, Rais Maduro alisema, “Kikosi chochote cha kijeshi duniani kinaelewa uwezo wa makombora ya Igla-S, na Venezuela inamiliki kwa uchache 5,000 ya aina hiyo.”

Makombora hayo ya Igla-S, yaliyoundwa kuangusha ndege zinazoruka masafa ya chini, yalitumika katika mazoezi ya kijeshi yaliyoamriwa na Maduro kujibu harakati za kijeshi za Marekani, zilizowakakasirisha viongozi wa nchi nyingi za Amerika Kusini.

Washington imetuma ndege za siri na meli za kivita katika visiwa vya Caribbean kama sehemu ya kile inachokiita juhudi za kukabiliana na mihadarati, na kuharibu meli zisizopungua nane ambazo ilidai zilikuwa zikisafirisha dawa za kulevya kutoka Venezuela kwenda Marekani.

Marekani imetuma jeshi kubwa katika Bahari ya Caribbean na maji katika pwani ya Venezuela tangu majira ya joto ya mwaka huu, na hivyo kuzua uvumi kwamba Trump ana mipango kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro, ambaye anakabiliwa na tuhuma za Washington kwamba anaunga mkono ugaidi na kuhusika na ulanguzi wa mihadarati nchini Marekani, madai ambayo yanatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa ni ya uongo yanayoilenga Venezuela na kiongozi wake kutokana na misimamo yake ya kupinga ubeberu wa Marekani. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *