Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 92 anaripotiwa kuwa karibu kushinda muhula wa nane madarakani, hali iliyochochea maandamano katika mji mkuu na miji mingine nchini humo kufuatia tuhuma za udanganyifu wa uchaguzi.

Baraza la Katiba limekataa maombi 10  yaliyokuwa na madai ya kujazwa kwa kura bandia, vitisho kwa wapiga kura, na dosari nyinginezo, likitaja sababu za ukosefu wa ushahidi wa kutosha au halina mamlaka ya kufuta uchaguzi. Maamuzi ya baraza hilo ni ya mwisho na hayawezi kukatiwa rufaa.

Issa Tchiroma, aliyekuwa mshirika wa Biya na sasa ni kiongozi wa upinzani, alidai kupitia ukurasa wake rasmi wa kampeni kuwa ameshinda uchaguzi kwa asilimia 54.8 ya kura, akidai kuwa matokeo hayo yanawakilisha asilimia 80 ya wapiga kura. Hata hivyo, alikataa kuwasilisha malalamiko yake kwenye Baraza la Katiba, akionya kuwa hatakubali matokeo mengine yoyote.

“Kwa watu wa Cameroon, walio wengi kwa kiasi kikubwa, hawatakubali kamwe uhalalishaji wa Baraza la Katiba kuhusu upotoshaji na ujazaji wa kura, kwani jambo hilo limefika katika uangalizi wa dunia nzima. Ndugu zangu wapendwa wa taifa hili, hali ni ya kutia wasiwasi. Hatutaruhusu ushindi wetu kuibiwa. Ikiwa wanapendelea kutishia utulivu na amani ya nchi badala ya kukubali kushindwa, tutajibu kwa msimamo wa amani wa wananchi.”

Hatma ya matokeo

Cameroon 2025 | Uchaguzi
Rais Paul Biya ameiongoza nchi hiyo ya Afrika ya Kati tangu mwaka 1982.Picha: Etienne Mainimo/IMAGO

Serikali imekanusha tuhuma za udanganyifu wa kura na kuwataka wananchi kusubiri matokeo rasmi. Maandamano ya hapa na pale yamezuka katika miji kadhaa baada ya matokeo ya awali yaliyoripotiwa na vyombo vya habari vya ndani kuonyesha Biya anaelekea kushinda.

Siku ya Jumatano mapigano yalizuka kati ya vikosi vya usalama na wafuasi wa Tchiroma katika miji ya Maroua na Garoua kaskazini mwa Cameroon. Vikosi vya usalama vilitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wakiandamana katika mji mkuu, Yaoundé na Garoua.

Rais Biya, ambaye ameiongoza nchi hiyo ya Afrika ya Kati tangu mwaka 1982, anaweza kuendeleza utawala wake hadi karibu na umri wa miaka 100 iwapo Baraza la Katiba litathibitisha ushindi wake baadae wiki hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *