Mkoa wa Arusha umeendelea kuonyesha dhamira ya kuitaka Ligi Kuu msimu ujao baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, kuipiga jeki timu ya Mbuni kwa kuichangia Sh13.5 milioni kwa ajili ya posho, motisha na maandalizi ya michezo ya Championship msimu huu.
Makala ametoa msaada huo leo, Oktoba 23, 2025, wakati alipokutana na wachezaji pamoja na viongozi wa Mbuni FC kwenye kikao maalum kilichofanyika jijini Arusha na kutangazwa rasmi kuwa mlezi wa timu hiyo.
Makalla amesema amekubali kuwa mlezi wa timu hiyo kufuatia ombi ambalo liliwasilishwa kwake na JWTZ Brigedi ya Kanda ya Kaskazini na kuweka wazi kuwa anataka kuona Mbuni FC inakuwa mfano wa mafanikio na kutinga Ligi Kuu Bara msimu ujao.
“Kuanzia leo mimi ni mlezi wa Mbuni FC, nataka kuona timu hii inapanda daraja, natoa Sh13.5 milioni kama motisha ya kuanza safari hiyo. Pia nitahakikisha kila mechi kunakuwa na bonasi,” amesema Makalla.
Aidha Makalla ameongeza kuwa timu hiyo sasa itakaa katika kambi ya kisasa yenye ghorofa, itakayokuwa na mazingira rafiki ambayo itawafanya wachezaji kupambana zaidi na kutimiza malengo ambayo yamewekwa.
Katika kuthibitisha dhamira yake, Makalla pia amekabidhi mchele kilo 200, mafuta ya kula pamoja na luninga mpya ambayo italetwa kambini kwa ajili ya matumizi ya kambi ya timu hiyo, hatua iliyopokelewa kwa shangwe na wachezaji na benchi la ufundi.
Mkuu huyo wa Mkoa, alisisitiza kuwa Arusha, kama mji wa Kimataifa wa utalii, unapaswa kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu ili kuunganisha michezo na utalii wa kimataifa kupitia Afcon 2027.
Kwa upande wake, Mwenyekiti msaidizi wa Mbuni FC, Felician Mashauri, amemshukuru RC Makalla kwa moyo wa upendo na kujitolea kwake, akisema msaada huo utaleta morali kubwa kwa wachezaji na kuimarisha ari ya ushindi.
“Tunashukuru sana Mkuu wa Mkoa kwa kuamua kuwa mlezi wetu. Fedha hizi na vitu vingine ulivyotupa vitasaidia sana katika maandalizi ya timu na kuongeza morali kwa wachezaji.
“Tunaahidi kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunapanda daraja na kuiwakilisha Arusha Ligi Kuu, kikubwa tu mashabiki watuunge mkono,” amesema Mashauri.
Mara baada ya kukabidhiwa msaada huo Mbuni FC ambao ndio vinara wa Ligi ya Championship msimu wa 2025/26 kwa alama sita baada ya kucheza mechi mbili, imeanza safari usiku huu kuelekea mkoani Njombe kwa ajili ya kucheza mchezo wa Ligi dhidi ya Hausung FC. Mchezo huo utapigwa Oktoba 25, mwaka huu katika uwanja wa Amani uliopo Njombe.