KILA shabiki wa Yanga ana presha na dakika 90 ngumu zijazo wakati timu hiyo ikijiandaa kwenda kukabiliana na Silver Strikers ya Malawi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania kufuzu makundi.
Wakati presha ikiwa juu kwa kila Mwanayanga, kule kambini kuna mambo matatu aliyoanza nayo Kaimu Kocha Mkuu, Patrick Mabedi raia wa Malawi huku akifahamu ili wafuzu makundi, lazima washinde kwa angalau tofauti ya mabao 2-0 baada ya ugenini kufungwa 1-0.
Kocha Mabedi ndiye aliyekabidhiwa hatma ya Yanga kwenda hatua ya makundi ya michuano ya CAF na timu inasaka rekodi ya kufuzu kwa mara ya nne mfululizo baada ya kufanya hivyo 2022-2023 (Kombe la Shirikisho), 2023-2024 na 2024-2025 (Ligi ya Mabingwa).
Mmalawi huyo alitangazwa kuchukua nafasi ya Romain Folz, ambaye uongozi wa Yanga ulisitisha mkataba wake Oktoba 18, 2025, saa chache baada ya kikosi hicho kufungwa bao 1-0 ugenini na Silver Strikers.
Katika kuhakikisha Yanga inafuzu makundi, Mabedi ambaye amewahi kusema anawafahamu vizuri wapinzani anaokwenda kukabiliana nao, kwanza anataka ukuta wake usiruhusu bao lolote akiwaandaa mabeki na viungo kukaba kwa nguvu na kwa nidhamu.
“Hatukuwa na nidhamu nzuri sana kwenye ulinzi ndio maana tuliruhusu lile bao, nimewaambia wachezaji wasirudie makosa yale, hii ni timu kubwa (Yanga) na wao ni wachezaji wakubwa,” amesema Mabedi.
“Tunatakiwa kucheza kwa nidhamu lakini wawe wakatili kutoruhusu wapinzani kujipanga na hata kukaribia lango letu, kama tutaruhusu bao tutazidi kujiweka kwenye presha.”
Aidha Mabedi amesema jambo la pili anataka kuona wachezaji wakimalizia nafasi ambazo watatengeneza kwa kuwa watahitaji kushambulia kwa nguvu.
Mabedi alisema Yanga haitakiwi kukaa nyuma na anataka kila nafasi ambayo wataitengeneza iwe kama haitapatikana tena ili wapate mabao ya haraka. Katika hilo, anakiandaa kikosi chenye uwezo wa kucheza kwa kasi muda wote wa mechi.
“Tupo nyumbani tutakuwa mbele ya mashabiki wetu tunaoamini watajaa uwanja mzima, tunatakiwa kuipigania klabu yetu, hapo ni muhimu kutangulia kupata mabao ya haraka.
“Tunatakiwa kuhakikisha tunakuwa na njaa ya kumalizia nafasi ambazo tutazingeneza, mpinzani anapofanya makosa tunatakiwa kumwadhibu na sio kumfanya ajipange upya.
“Hizi ni mechi kubwa, hatutakiwi kuidharau Silver Strikers, ina kocha na wachezaji wazuri lakini Yanga inaweza kuonyesha kuwa bora zaidi kwenye mchezo huu wa nyumbani ambao utaamua hatma yetu, tunatakiwa kumaliza mechi mapema,” amesema.
Mwanaspoti linafahamu jambo la tatu ambalo Mabedi ameanza nalo katika kikosi cha Yanga kuelekea mechi hiyo ni kubadili kikosi tofauti na kile kilichocheza mechi ya ugenini.
Mabadiliko ya kikosi hicho yanakuja kufuatia uwepo wa taarifa za kupona kwa mshambuliaji kinara wa Yanga msimu uliopita, Clement Mzize ambaye msimu huu amecheza mechi moja pekee ya kimataifa kati ya tatu.
Mzize aliyepata majeraha katika mechi ya kwanza dhidi ya Wiliete iliyochezwa Septemba 19, 2025 nchini Angola, huenda akaanza Jumamosi baada ya mahitaji ya Mabedi kutaka soka la kasi ambalo mshambuliaji huyo analiweza.
Wakati Mzize anauguza majeraha, alikosekana katika mechi nne za mashindano dhidi ya Pamba Jiji (Septemba 24, 2025), Wiliete (Septemba 27, 2025), Mbeya City (Septemba 30, 2025) na Silver Strikers (Oktoba 18, 2025). Kwa jumla, msimu huu Mzize ameanza mechi moja tu dhidi ya Wiliete iliyochezwa Septemba 19, 2025. Awali alitokea benchi katika Ngao ya Jamii dhidi ya Simba (Septemba 16, 2025).
Nyota huyo aliyeibuka kinara wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga 14, mawili nyuma ya kinara wa jumla, Jean Charles Ahoua, amekuwa na mchango mkubwa anapopata nafasi ya kuwepo kikosini kutokana na kasi na uwezo alionao wa kutokea pembeni akitengeneza nafasi kwa wenzake na kufunga mwenyewe.