Marco Rubio anaelekea Israel huu ukiwa ni mfululizo wa ziara za maafisa waandamizi wa serikali ya Rais Donald Trump nchini Israel. Ziara hiyo na za viongozi wengine waliotangulia wa Marekani zinalenga kudumisha usitishaji wa vita vilivyodumu kwa miaka miwili kati ya Hamas na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Kwenye ziara hiyo Rubio anatarajia kukitembelea kituo kipya cha kudumisha makubaliano kati ya Hamas na Israel kilicho chini ya Marekani.

Muda mfupi kabla ya kuanza safari yake Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Marekani hata hivyo alionya kuhusu hatua zinazofanywa na bunge la Israel zinazolenga kuutwaa Ukingo wa Magharibi. Rubio amesema hatua hizo zinauhatarisha mpango wa Trump wa kuvimaliza vita vya Gaza.

Marekani: Israel haitaunyakua Ukingo wa Magharibi

Naye Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance aliyekuwa Israel siku moja iliyopita ameikemea pia hatua hiyo na kusisitiza kuwa Israel haitalinyakua eneo hilo

Jumatano, Bunge la Israel lilipitisha miswada miwili inayolenga kuunyakua Ukingo wa Magharibi. Hatua hiyo imejiri wiki moja tu tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa Rais Donald Trump wa kusitisha vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.

Bunge la Israel lilipitisha miswada inayolenga kuunyakua Ukingo wa Magharibi
Bunge la Israel Picha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Katika hatua nyingine, Shirika linaloviwakilisha vyombo vya habari vya kimataifa nchini Israel na katika mamlaka ya Palestina FPA, limeelezea kusikitishwa kwake na kitendo cha Mahakama ya Juu ya Israel cha kuahirisha uamuzi wa ombi la kuwaruhusu waandishi wa habari wa kigeni kuingia Gaza mara moja.

Tangu vita vilipoanza Gaza Oktoba 2023 mamlaka za Israel zimekuwa zikiwazuia waandishi habari wa kigeni kuingia katika ukanda huo na kuwaruhusu baadhi yao chini ya udhibiti mkali. Chama hicho kiliwasilisha ombi la kutaka ruhusa ya kuingia Gaza baada ya makubaliano ya kusitisha vita.

Mahakama ya Israel ilizipa mamlaka husika mwezi mmoja wa kuandaa mpango utakaowapa ruhusa waandishi wa kigeni kuingia Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *