Zaidi ya siku 900 za mapigano makali zimesambaratisha maisha ya watu, zikiacha zaidi ya watu milioni 30 wakiwa wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku wanawake na watoto wakiwa katika hatari kubwa zaidi ya kuangamia.
Maisha ni changamoto kubwa yaonya IOM
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Operesheni wa Shirika la IOM, Ugochi Daniels, ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Sudan, ameelezea hali ya uharibifu mkubwa katika mji mkuu Khartoum na maeneo mengine.
“Kiwango hiki cha watu kurejea Khartoum ni ishara ya uimara, lakini pia ni onyo,” amesema. “Nilikutana na watu wanaorudi katika jiji lililojeruhiwa na vita, nyumba zikiwa zimeharibiwa na huduma za msingi hazifanyi kazi. Uthubutu wao wa kuanza upya ni wa kushangaza, lakini maisha bado ni changamoto kubwa.”
Daniels ameongeza kuwa kuenea kwa kipindupindu, homa ya kidingapopo na malaria kunasisitiza uharaka wa kurejesha maji safi, huduma za afya na huduma nyingine muhimu. “Ni hapo tu ndipo watu wataweza kuanza maisha upya kwa kweli,” amesema.

UNHCR: Huu ni moja ya mizozo mikubwa zaidi katika miongo kadhaa
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, Kelly T. Clements, janga la watu kufurushwa Sudan limefikia kiwango cha kutisha.
“Hii ni moja ya mizozo mikubwa zaidi ya ulinzi ambayo tumeishuhudia katika miongo kadhaa,” amesema baada ya kutembelea maeneo ya wakimbizi ndani na nje ya Khartoum.
“Mamilioni wamefurushwa ndani na nje ya nchi, na familia zinazorejea hazina msaada wowote. Nilizungumza na familia zilizokimbia Al Fasher zikiwa na simulizi za kutisha za kulazimishwa kuacha kila kitu nyuma na kuchukua njia hatarishi ili kunusuru maisha yao. Hali ni tete kila mahali, na msaada unahitajika kila upande.”
UNHCR imesisitiza kuwa ukarimu wa muda mrefu wa Sudan kwa takriban wakimbizi 900,000 sasa uko hatarini, huku hisia za chuki dhidi ya wageni zikiongezeka na kuhatarisha ulinzi wa walio hatarini zaidi.
UNICEF: Watoto wanakabiliwa na udhalilishaji
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Ted Chaiban, ameelezea mateso ya watoto kama “ukumbusho mkubwa wa kilicho hatarini.”
Amesema “Watoto wanadhoofika kwa utapiamlo, wanakabiliwa na vurugu, na wako katika hatari ya kufa kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika. Jamii nzima inapambana kuishi katika hali zinazodhalilisha utu.”
Chaiban amesisitiza kwamba uthabiti wa familia za Wasudan lazima ulinganishwe na mshikamano wa dunia.
“Familia zinaonesha ujasiri wa ajabu katikati ya mateso yasiyofikirika,” amesema. “Dunia lazima ichukue hatua za haraka kuhakikisha upatikanaji wa huduma, rasilimali, na hatimaye kusitisha vita.”

Msaada wa dharura unasambazwa katika Bandari ya Sudan kwa watu waliokimbia migogoro katika maeneo mengine ya Sudan.
WFP: Nimeona tumaini katikati ya magofu
Licha ya changamoto kubwa, mashirika ya misaada yanaendelea kutoa huduma kadri ya uwezo wao.
Mkurugenzi Msaidizi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Chakula Duniani WFP, Valerie Guarnieri, amesimulia alichoshuhudia Khartoum, “Niliona jiji lililoharibiwa na vita, ambapo familia zinazorejea nyumbani zinahitaji chakula, maji na huduma za msingi kwa dharura. Lakini zaidi ya yote, niliona azma na matumaini ya kuanza maisha upya. Niliona matumaini.”
Guarnieri amesema WFP inashirikiana na mashirika ya ndani kusaidia familia zilizofurushwa, wakazi na wanaorejea kwa kuwapatia chakula, lishe, milo ya wanafunzi shuleni na kusaidia kurejesha huduma muhimu.
Wito wa kusitishwa mapigano na upatikanaji wa misaada haraka
Mashirika hayo manne yameomba kusitishwa kwa mapigano mara moja, upatikanaji usio na vikwazo kwa misaada ya kibinadamu, na ufadhili wa haraka ili kudumisha shughuli za uokoaji maisha.
Mpango wa Hatua za Kibinadamu wa 2025 kwa Sudan unahitaji dola bilioni 4.2 lakini umefadhiliwa kwa asilimia 25 pekee, hali inayotishia kuzuia msaada muhimu kwa mamilioni ya watu.
Katika tamko la pamoja, mashirika hayo yamesema “IOM, UNHCR, UNICEF na WFP yanathibitisha dhamira yao ya kusimama na watu wa Sudan. Lakini jumuiya ya kibinadamu haiwezi kutenda peke yake dunia lazima ichukue hatua sasa ili kuzuia janga kubwa zaidi la kibinadamu.”