Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka vijana nchini, wasidanganywe na nia ovu…Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka vijana nchini, wasidanganywe na nia ovu…

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka vijana nchini, wasidanganywe na nia ovu zinazotangazwa mitandaoni, akisema Tanzania ni nchi salama na inawategemea.

Katika msisitizo wake, Dkt Samia amesema hakuna mwingine mwenye hatimiliki ya Tanzania zaidi ya vijana, hivyo wanapaswa kutuliza kile alichokiita munkari kwa maslahi na ustawi wa Taifa.

Dkt Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Oktoba 23, 2025 alipozungumza katika mkutano wake wa kuhitimisha kampeni za urais, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.

“Vijana wa Tanzania msidanganywe, ukichukua Afrika Mashariki pengine na Kusini kidogo na kati Tanzania ni pepo. Hapa upo kwenye nchi yenye jina, yenye sifa zake, yenye kuendeleza watu wake, msidanganywe. Wale walioko nje huko wasiwadanganye, hapa mpo pazuri kweli kweli.

“Ukipata fursa ya kuingia tu kwa majirani zetu hapo, mkaangalie vijana wenzenu wanavyokula ngumu, utasema narudi Tanzania ndio kwetu,” amesema.

Amewasisitiza vijana kuwa ndio wenye mamlaka na nchi na wanategemewa kuiendeleza kwa namna ambavyo waasisi waliiendeleza hadi ilipofika sasa.

“Niwaombe sana vijana tulizeni munkari, kaeni vizuri, hii nchi ni mali yenu wala si mali ya mwingine. Hakuna mwenye cheti anayesema hii nchi ni mali yangu.

“Sisi wazazi wenu tunapita, nchi hii inawategemea ninyi, tunatarajia tuwaachie nchi hii muiendeshe kama tunavyoiendesha hivi. Kwa hiyo vijana wa Tanzania msidanganywe hata kidogo,” amesema.

#StarTvUpdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *