Haya yalifanyika wakati viongozi walipokuwa wakikusanyika kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Misri huko mjini Brussels.
Mikataba kadhaa ya mikopo imetiwa saini ukiwemo mkataba mmoja wa mkopo wa yuro bilioni 4 kama msaada wa Ulaya kwa Cairo.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wakati alipokuwa akimpokea Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema kuwa, watatia saini mikataba kadhaa itakayofungua njia za biashara nchini Misri.
Yuro milioni 200 kwa ajili ya uhamiaji
Mnamo Disemba mwaka jana, Umoja wa Ulaya ulitoa awamu ya kwanza ya yuro bilioni moja kwa Misri na kufikisha kiasi cha msaada jumla wa kifedha kufikia dola bilioni tano.
Mikataba hiyo inafuatia ushirikiano wa kimkakati uliotiwa saini Machi mwaka jana wakati ambapo Umoja wa Ulaya unalenga kujenga uhusiano mzuri na Misri ambayo ni mshirika muhimu Mashariki ya Kati.
Umoja wa Ulaya pia umezindua yuro bilioni 1.8 za uwekezaji kwa ushirikiano na taasisi nyengine za kifedha Ulaya pamoja na yuro milioni 600 kama msaada unaolenga miradi maalum ambapo yuro milioni 200 zitatumika kudhibiti uhamiaji.
“Nguzo ya nne ni kuhusu uhamiaji. Misri imeonesha ukarimu wa hali ya juu kwa kuwahifadhi mamilioni ya wahamiaji na wakimbizi. Ushirikiano wetu katika uhamiaji unahusu maeneo yote. Ushirikiano huu uko chini ya yuro milioni 200 za msaada wa Umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka miwili ijayo na tutashirikiana kupambana na walanguzi,” alisema Von der Leyen.
Ufadhili wa ujenzi mpya wa Palestina
Kwa upande wake Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi amesema suluhisho la uhamiaji ni kufanya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kisiasa na kiusalama na kubuni ajira za kutosha na kutoa mafunzo ya kazi, hiyo ikiwa kama kuweka msingi wa suluhisho la suala la uhamiaji.
“Kutokana na hili, nathibitisha kwamba Misri ina jukumu muhimu katika kuzuia uhamiaji haramu. Tulizuia kuondoka kwa boti zozote kutoka Misri kuanzia Septemba 2016. Na Misri wakati huu, inawapa hifadhi zaidi ya wakimbizi milioni 9.5 ambao wamewasili Misri wakikimbia migogoro katika nchi zao,” alisema Al-Sissi.
Von der Leyen pia ametangaza mpango wa kikundi cha ufadhili wa Palestina kitakachowaleta pamoja washirika wa kimataifa kwa ajili ya kuleta mageuzi na ujenzi mpya wa Gaza. Amesema juhudi za Misri za upatanishi na mpango wa mkutano wa ujenzi mpya wa Gaza utakuwa muhimu.
Makubaliano yote hayo yametiwa saini na Kamishena wa Uchumi wa Umoja wa Ulaya Vladis Dombrovskis na waziri wa mipango wa Misri Rania Al-Mashat.