Rais wa China Xi Jinping alizindua Mpango wa Uongozi wa Kimataifa (Global Governance Initiative) katika Mkutano wa hivi karibuni wa Ushirikiano wa Shanghai (Shangai Cooperation Organisatio), akiuwasilisha kama mfumo mpya wa ushirikiano wa kimataifa wa haki na shirikishi zaidi.
China inajitambulisha kama ‘mwanamageuzi’ na ‘mlinzi’ wa mfumo wa dunia, China inawasilisha mpango wa GGI kama nguzo ya nne kuu ya sera za kigeni baada ya Mpango wa Maendeleo ya Ulimwenguni, Mpango wa Usalama wa Ulimwenguni na Mpango wa Ustaarabu wa Ulimwenguni.
Huku kukiwa na mashaka ya kijiografia na kuporomoka kwa imani katika mifumo ya nguvu za jadi, China imewasilisha maono yake ya dunia yenye usawa zaidi kupitia mpango huu.
Mpango wa GGI inafafanua upya kanuni zinazoongoza mahusiano ya kimataifa. Inategemea dhana kuu tano: uhuru wa nchi, kuheshimu sheria za kimataifa, uhusiano wa kweli wa pande nyingi, mtazamo unaohusisha raia watu katikati na kufanya kazi kwa ajili ya matokeo halisi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, mawazo haya hayakusudiwi kubadilisha mfumo uliopo, bali kuboresha taasisi za kimataifa ziwe za uwakilishi mpana zaidi, zenye ufanisi na usawa.
Lengo kuu la mpanfo wa GGI ni kuboreshwa kwa mfumo wa taasisi za dunia kwa kuondokana na upendeleo wa upande mmoja na migawanyiko ya kiitikadi.
Uanzishwaji wa mpango wa GGI unaonyesha utambuzi kwamba mfumo wa sasa ulioundwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia hauwezi tena kushughulikia changamoto tata za leo kama vile mabadiliko ya tabianchi, usimamizi wa kidijitali, na ukosefu wa usawa wa kiuchumi.
China inasisitiza kuwa hakuna taifa moja linalopaswa kutawala mchakato wa mageuzi, na kwamba mataifa yote – makubwa au madogo, tajiri au maskini – yanastahili sauti katika kuunda mustakabali wa dunia.
Wakati muafaka wa mageuzi
Uzinduzi wa mpango wa GGI unakuja wakati muhimu – mwaka 2025 ukiadhimisha miaka 80 ya Umoja wa Mataifa (UN), kipindi cha kujitafakari kimataifa.
Mpango wa GGI unaibua ukweli kwamba taasisi zilizoundwa baada ya 1945 hazina tena uwezo wa kushughulikia changamoto nyingi za karne ya 21.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa mfano, mara nyingi limekwama kutokana na mamlaka ya kura ya turufu ya wanachama watano wa kudumu, jambo linalolizuia kushughulikia migogoro mikubwa kama vita vya Urusi na Ukraine au mauaji ya halaiki ya Israel huko Gaza.
Hali hii imezidisha hasira za kimataifa na wito wa mageuzi.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, kwa muda mrefu amesisitiza kuwa UN lazima ikuwe na kutosalia tu mikonini mwa mamlaka finyu ya waanzilishi wake, akijulikana kwa kauli yake maarufu: “Dunia ni kubwa kuliko nchi tano.”
Maoni haya yanaendana na yale ya Mpango wa GGI wa China, ambayo pia unalenga kujenga mfumo shirikishi zaidi.
Shirika la Biashara Duniani (WTO), ambalo hapo awali lilikuwa kiini cha ushirikiano wa kiuchumi, limepoteza ushawishi kutokana na migogoro kati ya mataifa makubwa na kushindwa kwake kusasisha kanuni za biashara.
Wakati huo huo, kuporomoka kwa mikataba muhimu ya kudhibiti silaha kama INF, na kudhoofika kwa mikataba ya kuzuia uenezaji wa silaha, kumezua hofu ya nchi nyingi kutafuta silaha mpya.
Katika mazingira ya pengo la uongozi na lenye uhalali, Mpango wa GGI wa China unapata uzito kwa kukuza mazungumzo na usalama wa pamoja kama mbadala wa ushindani wa aina ya Vita Baridi.
Kisiasa, ujumbe ni wazi. Marekani, chini ya sera ya “Marekani Kwanza” ya Donald Trump, inaendelea kujiondoa katika wajibu wa kimataifa, wakati Beijing ikijitokeza kujaza pengo hilo.
Mpango wa GGI haudai kuunda mfumo mbadala, bali kuimarisha mfumo uliopo kwa kushughulikia masuala matatu makuu: kutowakilishwa kwa mataifa yanayoendelea (Global South), kudhoofika kwa mamlaka ya Umoja wa Mataifa na utekelezaji duni wa sera za kimataifa
Ujumbe wa msingi ni kwamba uongozi wa dunia hauwezi tena kuwa haki ya wachache, bali lazima ubadilike kuakisi hali halisi ya dunia yenye kuwakilishwa na mataifa mengi yenye nguvu(multipolar world).