MSIMU wa tatu wa Zanzibar Half Marathon unatarajiwa kufanyika Novemba 30, 2025, ukiwa na lengo la kurejesha matumaini kwa mama aliyeathirika na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani waliotelekezwa na wenzi wao baada ya kujifungua ambapo katika mbio hizo, mshindi wa kwanza kilomita 21, atazawadiwa Sh6 milioni.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake Migombani Mjini Unguja.

Amesema, kupitia mbio hizi, jamii inahamasishwa kujenga mioyo wa huruma, mshikamano na uwajibikaji wa malezi ili kuwa na familia bora zenye kupendana.

“Ifikapo Novemba 30, 2025 kutafanyika msimu wa tatu wa mbio za Stop GBV Half Marathon Mji Mkongwe Zanzibar kuanzia asubuhi, hivyo nawaomba wananchi washiriki mashindano hayo yenye lengo la kutoa matumaini kwa mama aliyeathirika na vitendo vya ukatili,” amesema kiongozi huyo.

Amesema, mbio hizo zinatambuliwa kimataifa na zipo katika kalenda ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi. 

Naye, Mwenyekiti wa Asma Mwinyi Foundation na mwanzilishi wa mbio hizo, Asma Ali Mwinyi amesema mbio hizo zitashirikisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali katika mbio za umbali wa kilomita 5, 10 na 21, ambazo ndio zilizojipatia umaarufu ndani na nje ya Zanzibar .

Ameeleza, washiriki wa mbio za Stop GBV Half Marathon watapata zawadi za ushindi kwa wanaume na wanawake ambapo mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21 atavuna Sh6 milioni, wa pili Sh3.5 milioni, watatu Sh2.5 milioni, wanne Sh1.5 milioni, watano Sh1 milioni. Kuanzia nafasi ya sita hadi kumi kila mmoja atapatiwa Sh100,000.

Kwa upande wa mbio za kilomita 10, mshindi wa kwanza atazawadiwa Sh1.5 milioni, wapili Sh1.3 milioni, watatu Sh1 milioni, wanne Sh700,000 na watano Sh500,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Uhifadhi wa Mji Mkongwe, Ali Bakar, amesema amekuwa na ushirikiano ya karibu katika kuendeleza Tamasha hilo ambalo linatarajiwa kufanyika katika kuelekea kilele cha kuanzimisha siku ya Mji Mkongwe kila ifikapo Desemba 2, siku ambayo iliasisiwa na kupewa hadhi ya urithi wa dunia Mji huo.

Amesema tamasha hilo la msimu wa tatu licha ya kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji, pia itakuwa ni fursa ya kuutangaza mji mkongwe kiutalii sambamba na wafanyabiashara wadogo wadogo kupata fursa ya kufanya bishara zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *