DEREVA chipukizi kutoka Morogoro, Waleed Nahdi ambaye amekuwa tishio jipya kwenye mbio za magari kuwania ubingwa wa taifa mwaka huu, amesema anaamini atashinda za Guru Nanak, zitakazofanyika Novemba 8, 2025 katika eneo la Makuyuni, Magharibi mwa Jiji la Arusha.

Akiwa na pointi 80 kibindoni, Nahdi yuko nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa wazoefu, Randeep Singh na Ahmed Huwel, ambaye amekamata usukani wa mbio hizi za ubingwa wa Taifa kwa mwaka huu.

“Hivi sasa najiogopa mwenyewe, nimeanza rasmi mwaka huu na nimepanda juu ghafla hivi. Najiona ni bingwa kwa mwaka huu,” amesema Nahdi wakati akiandaa gari lake kwa ajili ya mbio hizo.

“Siamini niko juu ya magwiji kama Manveer Birdi, Gupal Sandhu na Sameer Shanto ambao wako kwenye fani kwa zaidi ya miongo miwili. Hii inanipa changamoto ya kuzidi kufanya vizuri,” amesema Nahdi ambaye huendesha gari aina ya Subaru Impreza N11.

Dereva huyu chipukizi amesema mafanikio kwake yamekuja haraka kuliko ilivyotarajiwa kwani ameanza rasmi kuingia mchezoni mwaka huu.

MAG 01

“Namshukuru sana msoma ramani Awadh Bafadhil ambaye uzoefu wake wa zaidi ya miaka 20 katika fani umechangia sana katika kuboresha uwezo wangu wa kuendesha gari ya mashindano kwa usahihi kutokana na maelekezo ya usomaji wake,” amesema.

Katika raundi ya hitimisho, Huwel alijikusanyia jumla ya pointi 105, akianza na pointi 35 (30+5) baada ya kushinda Mkwawa Rally, Agosti 2025 kabla ya kutwaa pointi 70 (60+10) kwa kushinda Mkwawa Rally of Tanzania mwishoni mwa juma.

Randeep Singh ni wa pili akiwa na jumla ya pointi 88 na alianza na pointi 35 (30+5) kwa kushinda raundi ya pili Dar es Salaam na aliongeza pointi 15 (11+4) katika raundi ya tatu kabla ya kutwaa pointi 38 (30+8) katika mbio za Mkwawa Rally of Tanzania akifuatiwa na Nahdi , kisha nafasi ya nne imekamatwa pia na dereva kutoka Morogoro, Samir Shanto mwenye pointi 74.

Dereva kutoka Arusha, Gurpal Sandhu ni wa tano akibeba bango la pointi 73 mbele ya bingwa mtetezi Manveer Birdi nafasi ya sita akitwaa jumla ya pointi 62.

Dereva kutoka Dar es Salaam, Shehzad Munge anashika nafasi ya saba akiwa na pointi 62 akimwacha Prince Charles Nyerere wa Arusha mwenye pointi 40, kwa pointi 22.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *