Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ametoa ripoti yake mpya kuhusu mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni Israel katika Ukanda wa Gaza, na kutoa maelezo ya kina kuhusu ushiriki wa kimataifa katika ukatili wa Tel Aviv.

Toleo la mapema la ripoti hiyo, yenye jina la Mauaji ya Kimbari ya Gaza: Uhalifu wa Pamoja lilichapishwa jana Jumatano. Albanese amesema katika ripoti hiyo kuwa kuendelea kwa uharibifu wa maisha ya Wapalestina katika eneo la pwani kumewezeshwa kupitia njia za kijeshi, kiuchumi, kidiplomasia na hata zile zinazoitwa za kibinadamu za mataifa ambayo mara kwa mara yametanguliza mbele maslahi ya kisiasa na kimkakati kuliko haki za binadamu.

Amesema, kidiplomasia, madola ya Magharibi, yakiongozwa na Marekani na Umoja wa Ulaya, yamekuwa yakiukingia kifua mara kwa mara utawala wa Israel dhidi ya uwajibikaji.

“Maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kutaka kusitishwa mapigano yamepigiwa kura ya turufu au kudhoofishwa, huku ukatili wa kijeshi wa utawala wa Israel ukitajwa kama “kujilinda halali,” amesema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa.

Francesca Albanese ameongeza kuwa, misaada ya kijeshi pia imekuwa na nafasi kubwa katika kuendeleza mauaji ya kimbari huko Gaza. 

Muaji ya kimbari ya Israel huko Gaza

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema, Ujerumani, Uingereza, India, Italia, Ufaransa, Uhispania na kadhalika zimechangia silaha na teknolojia ambayo imechochea moja kwa moja mashambulizi ya kijeshi huko Gaza.

Ripoti hiyo amesema: Licha ya mauaji ya kimbari yaliyofanyika huko Gaza, biashara na serikali ya Israel iliongezeka mwaka 2024, huku Ujerumani (+$836 milioni), Poland (+$237 milioni), Ugiriki (+$186 milioni), na hata mataifa ya Kiarabu kama UAE (+$237 milioni) na Misri (+$199 milioni) yakichochea zaidi uaduii wa utawala huo.

Albanese pia amekumbusha kwamba utawala wa Isarel na Marekani ziliunda kinachojulikana kama Taasisi ya Masuala ya Kibinadamu ya Gaza, mfumo wa misaada ya kijeshi ambao ulipelekea kuuawa zaidi ya raia 2,000 katika vituo vya usambazaji wa chakula huko Gaza kati ya Machi na Julai 2025.

Karibu Wapalestina elfu 70 wameuawa katiika kampeni ya mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza ikisaidiwa kwa hali na mali na madola ya Magharibi. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *