Shirika la Reli Tanzania (TRC) limetoa taarifa ya kurejea kwa huduma za usafiri wa treni za SGR baada ya hitilafu iliyotokea mapema leo, likiwahakikishia wananchi kuwa usafiri unaendelea kama kawaida.
Kupitia taarifa yake kwa umma, TRC imewaomba radhi wateja wake kwa usumbufu uliotokana na tukio hilo na kuwashukuru kwa uvumilivu waliouonyesha wakati huduma zilipokatizwa kwa muda mfupi.
Awali, kulikuwa na ajali ndogo ya treni ya abiria aina ya EMU iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma majira ya saa mbili asubuhi, baada ya hitilafu za uendeshaji katika eneo la Ruvu, mkoani Pwani. Kwa mujibu wa taarifa za TRC, hakuna madhara makubwa yaliyoripotiwa kufuatia tukio hilo.
Timu ya wataalamu ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama, ilifika haraka eneo la tukio kufanya uchunguzi na kuhakikisha huduma zinarejea kwa usalama.
TRC imesisitiza kuwa huduma zote za SGR sasa zinaendelea kama kawaida na imewahakikishia abiria usalama na ufanisi katika safari zote zijazo.
#Azamtvupdates
✍ Warda John
Mhariri | @claud_jm