
BAADA ya TRA United zamani Tabora United jana kushindwa kufungana na maafande wa Mashujaa FC kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mkoani Tabora, timu hiyo imefikisha mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya kuonja ladha ya ushindi.
Sare hiyo ya jana ni ya tatu mfululizo kwa kikosi hicho msimu huu wa 2025-2026, ingawa rekodi ya kucheza mechi hizo 11 bila ya ushindi ni kuanzia msimu uliopita wa 2024-2025, ikiwa ni mwendelezo mbaya wa timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.
Mara ya mwisho kwa timu hiyo kushinda katika Ligi Kuu Bara, ilikuwa ushindi wa bao 1-0, la kujifunga kutoka kwa Mganda, Dissan Galiwango wa Dodoma Jiji dakika ya 35, Februari 28, 2025. Kuanzia hapo hadi leo kikosi hicho hakijashinda tena.
Katika mechi hizo 11 za Ligi Kuu Bara ambazo timu hiyo haijashinda kuanzia msimu uliopita hadi sasa, imepoteza saba na kutoka sare minne, imefunga mabao manne, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 21.
Timu hiyo msimu uliopita, ilifundishwa na makocha wanne, akianza Mkenya, Francis Kimanzi, kisha Mkongomani Anicet Kiazayidi anayeifundisha Azam akiwa msaidizi wa Florent Ibenge, baada ya kuondoka akatua Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe.
Hata hivyo, Aprili 18, 2025, uongozi wa TRA ukamtangaza Kocha, Mzambia Simonda Kaunda kuchukua nafasi ya Mangombe, hadi mwisho wa msimu wa 2024-2025, akizifundisha Nkana, Forest Rangers, Chambishi FC na Roan United FC zote za kwao Zambia.
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo msimu huu, Kocha wa TRA United, Mkenya Kassim Otieno amesema licha ya kuanza kwa sare katika mechi tatu mfululizo, lakini bado anaendelea kutengeneza kikosi cha ushindani, kwa sababu wengi wao ni wapya.