Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limerejesha safari za treni za umeme za SGR, baada ya kusitisha kwa muda leo.

Hatua hiyo imekuja baada ya matengenezo ya muda mfupi yaliyofanyika, kutokana na treni ya Electric Multiple Unit – EMU maarufu mchongoko iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 kupata ajali katika kituo cha Ruvu mkoani Pwani.

Taarifa kwa umma iliyotolewa mchana huu na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala imeeleza kuwa safari sasa zinaendelea kama kawaida.

“Shirika la Reli Tanzania linapenda kuujulisha umma kuwa huduma za usafiri wa treni za SGR zimerejea na kuendelea kama kawaida. Shirika linaomba radhi wateja wake kwa usumbufu uliojitokeza na pia linawashukuru kwa uvumilivu wao. Huduma bora kwa wateja wetu ndiyo kipaumbele cha Shirika,” imeeleza taarifa hiyo.

Awali taarifa iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa umma ilitaja chanzo cha awali cha ajali hiyo huku ikieleza jitihada zinazofanyika sasa kuhakikisha huduma zinarejea.

“Shirika la Reli Tanzania (TRC) linautaarifu umma kuhusu ajali ya treni ya EMU iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma majira ya saa 2:00 asubuhi Oktoba 23, 2025 kutokana na hitilafu za kiuendeshaji, tukio hili limetokea kituo cha Ruvu na kwa taarifa za awali hakuna tukio la kifo.

“Timu ya wataalamu ikiongozwa na Katibu Mkuu Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu TRC, vyombo vya ulinzi na usalama na menejimenti ya TRC inaendelea na uchunguzi wa kina na juhudi za kuhakikisha kwamba huduma zetu zinarejea haraka,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa.

Treni ya mchongoko, ambayo imekuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma ilianza kutoa huduma Novemba Mosi, mwaka 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *