Dodoma/Dar. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema hakuna treni itakayoruhusiwa kuanza safari kwa sasa mpaka pale watakapotoa taarifa mpya.

Hatua hiyo imefuata baada ya treni ya Electric Multiple Unit (EMU) maarufu kama treni ya mchongoko iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 kupata ajali katika kituo cha Ruvu mkoani Pwani.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala amesema kwa sasa bado wanasubiriwa mafundi ili waweze kutoa taarifa mpya.

“Tupo eneo la tukio tunawasubiri mafundi ili waseme tatizo liko kwa kiasi gani, sababu hii ni ajali kama ajali zingine zinavyotokea.

“Hivyo mpaka sasa hakuna treni iliyoruhusiwa kuanza safari mpaka pale mafundi watakapotoa taarifa mpya. Muda rasmi wa kuanza safari hatujajua maana mafundi bado hawajatoa taarifa yoyote mpya,” amesema Mwanjala.

Awali, taarifa iliyotolewa kwa umma na TRC ilitaja chanzo cha awali cha ajali hiyo huku ikieleza jitihada zinazofanyika sasa kuhakikisha huduma zinarejea.

“Shirika la Reli Tanzania (TRC) linautaarifu umma kuhusu ajali ya treni ya EMU iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma saa 2:00 asubuhi Oktoba 23, 2025 kutokana na hitilafu za kiuendeshaji, tukio hili limetokea kituo cha Ruvu na kwa taarifa za awali hakuna tukio la kifo.

“Timu ya wataalamu ikiongozwa na Katibu Mkuu Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu TRC, vyombo vya ulinzi na usalama na menejimenti ya TRC inaendelea na uchunguzi wa kina na juhudi za kuhakikisha kwamba huduma zetu zinarejea haraka,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa.

Treni ya mchongoko, ambayo imekuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma ilianza kutoa huduma Novemba Mosi, mwaka 2024.

Safari za Treni ya SGR kutoka Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam, nazo zimesitishwa kwa muda leo asubuhi kufuatia ajali iliyotokea katika eneo la Ruvu, mkoani Pwani na kuwalazimu mamia ya abiria kusubiri kwa muda usiojulikana.

Abiria walioko katika Stesheni ya Magufuli wamesema tangazo lililotolewa na uongozi wa reli lilieleza kuwa mafundi wako kazini kurekebisha hitilafu, lakini halikufafanua ni lini safari zitaanza tena.

Anastazia Njenge, amesema ameamua kuondoka kituoni na kuelekea uwanja wa ndege baada ya kukosa taarifa za uhakika kuhusu muda wa kuondoka kwa treni.

“Kwa kuwa hakuna maelezo yaliyonyooka kama tutaondoka au la, nimeamua kwenda uwanja wa ndege kwa sababu nina kikao saa tisa alasiri na nimekuja hapa tangu saa mbili asubuhi lakini hadi saa sita mchana sioni muelekeo wa kike walichoeleza,” amesema Anastazia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *