Vikwazo hivyo dhidi ya Urusi vimewekwa huku Trump akilalamika kuwa mazungumzo yake na Rais wa Urusi Vladimir Putin yanayolenga kuvimaliza vita vya Ukraine hayazai matunda.

Hatua iliyotangazwa na Marekani Jumatano dhidi ya makampuni ya mafuta ya Urusi ya Rosneft na Lukoil imechukuliwa baada ya miezi kadhaa ya wito wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kumtaka Trump aiwekee Urusi vikwazo vikubwa zaidi katika sekta ya mafuta ya nchi hiyo.

Marekani imeiwekea Urusi vikwazo hivyo wakati Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte akiwa mjini Washington kwa mazungumzo na Trump. Rutte amesema kuwa Putin atakubali kusitisha vita na Ukraine ikiwa tu ataendelea kushinikizwa.

Muda mfupi baada ya Marekani kutangaza hatua hiyo, Urusi kupitia Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova imesema vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya sekta yake ya mafuta ni hatua isiyo na tija na inahatarisha juhudi za kidiplomasia za kuvimaliza vita vya Ukraine.

Urusi yalaani vikwazo vya Marekani

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Rais wa Urusi Dmitry Medvedev ameeleza mapema Alhamisi kuwa uamuzi wa utawala wa Trump wa kuufuta mkutano wa Budapest na kuweka vikwazo dhidi ya makampuni ya mafuta ya Urusi unaonesha kuwa Marekani ni adui wa taifa hilo na iko mbioni kuingia vitani na Moscow.

Medvedev amekosoa vikali vikwazo vya Marekani dhidi ya sekta ya mafuta ya Urusi
Aliyewahi kuwa Rais wa Urusi Dmitry MedvedevPicha: Yekaterina Shtukina/TASS/ZUMA/picture alliance

Aidha, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameipongeza hatua iliyochukuliwa na Marekani akiitaja kuwa ni hatua muhimu. Zelensky amesema uamuzi huo ni ishara muhimu kwa nchi nyingine duniani kuungana kuiwekea Moscow vikwazo.

Naye Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas umeupongeza utawala wa Trump kwa vikwazo dhidi ya sekta ya nishati ya Urusi na kuongeza kuwa ni ishara muhimu.

Hayo yanajiri wakati ambapo Umoja wa Ulaya katika hatua tofauti umekubaliana kuchuka hatua mpya dhidi ya Urusi zinazolenga kuyadhoofisha mapato ya Urusi yanayotokana na gesi na mafuta.

Itakumbukwa kuwa viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kufanya mkutano mjini Brussels Alhamisi huku moja ya ajenda yao ikiwa ni kujadili namna ya kuisaidia zaidi Ukraine katika mzozo wake dhidi ya Urusi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *