c

Chanzo cha picha, Reuters

Wanasiasa hawajawahi kuacha kuwashangaza wananchi. Kabla hatujayazungumza yanayotokea Zanzibar, nikupe ahadi iliwaacha wengi vinywa wazi na kuzusha mjadala kwenye bara la watu bilioni 1.5, Afrika.

Wiki kadhaa nyuma, mgombea wa kiti cha urais kupitia Uganda’s Common Man’s Party (CMP) Mubarak Munyagwa, ameahidi kuwa atapiga marufuku lugha ya Kiswahili, na badala yake ataikumbatia lugha ya Kifaransa.

Ahadi hii ilishangaza wengi, kwa kuzingatia kuwa Kiswahili kinazungumzwa Uganda na kinaunganisha wakaazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali.

Wakati Tanzania ikielekea katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, kuna ahadi za wagombea urais ambazo huzusha mijadala miongoni mwa wananchi. Mijadala hii huibuka kwa sababu ahadi hizi huonekana ni ngumu kutekelezeka au ni vituko.

Pande zote mbili za Muungano, yaani Zanzibar na Tanzania bara, kumeibuka wanasiasa wenye ahadi za aina hii. Lakini makala haya yana lengo la kuzipitia ahadi tano tu zilizozua mjadala kwa upande wa Zanzibar.

Pia unaweza kusoma

Usipooa wake wengi kifungo

fdc

Chanzo cha picha, Mwananchi

Mgombea Urais kwa tiketi ya NRA Zanzibar, Khamis Faki Mgau ameahidi kuwawezesha vijana kuoa wake zaidi ya mmoja pamoja na kuwalipa mshahara ili waweze kujikimu kimaisha.

Tatizo limeibuka pale aliposema, “vijana wakae tayari, nitakapo kuwa rais Zanzibar, ni marufuku kijana kuwa na mke mmoja, tunaanza na wake wawili kwenda mbele, na kijana ambaye hataoa wake wawili ni kifungo cha miaka sita.

Amefafanua ahadi yake kwa kusema, “kwa sababu nimejipanga kuwa mtoto kuanzia miaka mitano na kuendelea, tutakuwa tunawalipa mishahara. Nimedhamiria kila mwananchi, hasa vijana, kima cha chini cha mshahara ni laki 9. Nitawalipa. Nawaambia vijana atakeoa ni kuanzia wake wawili, asiyekubali kuoa wake zaidi ya wawili ni kifungo miaka sita.”

Mwinyi aendelee

DFX

Chanzo cha picha, Mwananchi

Wanasiasa na wataalamu wa siasa, husema lengo kuu la chama cha siasa ni kushika madaraka, lakini hilo ni tofauti kwa Mgombea Urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Kupitia Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib, ambaye anampigia debe Mgombea wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Hussein Ali Mwinyi achaguliwe tena.

“Kwa sababu tumeridhika na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na rais aliyopo madarakani, tunamuhitaji aendelee kufanya kazi, ili kuwaleta maendeleo Wazanzibari.” Ameweka wazi kuwa, “nikishinda urais sitouacha, lakini kwa hali ya chama chetu, tunataka Mwinyi aendelee tena kuwatumikia Wazanzibari.”

Juma amesema yeye anajiandaa kwa nafasi ya pili ili awe Makamo wa kwanza wa Rais ili amsaidie kazi Mgombea huyo atakapo chaguliwa kua rais tena.

Kulewa kwa leseni

c

Chanzo cha picha, IPPMEDIA

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Said Soud Said, ameweka ahadi endapo atapata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar kuwa Rais, watu wanaotaka kunywa pombe watatakiwa kuwa na leseni ili kujenga nidhamu kwa Wazanzibari na kwa yule atakayekiuka atapelekwa chuo cha mafunzo kwa miezi 3.

Ieleweke kuwa kwa Zanzibar chuo cha mafunzo sio kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, bali ni gereza. Kwa lugha nyingine ni kwamba mlevi asiye na leseni atakwenda gerezani kwa miezi mitatu.

Said anasema, “watu walewe kwa leseni ili askari wapate nafasi ya kuwalinda na kuwapeleka majumbani kwao au kuwaweka vituoni hadi waleuke, ndipo wawaache wende zao.”

“Haiwezekani tu mtu na pesa yake alewe, kisha apite akitukana au kumwaga mikojo .Eti kwa sababu ana pesa. Nchi lazima irudi kwenye nidhamu. Mtu akionekana kalewa, ataulizwa ‘una leseni? Kama hana, anakwenda miezi mitatu chuo cha mafunzo, akajirekebishe,” amefafanua.

Vitanda sita kwa sita marufuku

Kwa mara nyingine, yule yule Said Soud, amesema endapo atapata ridhaa ya wananchi wa Zanzibar, atapiga marufuku vitanda vya 6 kwa 6, kwani vinasababisha watu kutozaa. Akiwa rais mafundi watatakiwa kutengeneza vitanda visivyozidi futi 4 ambavyo vitachangia watu kuzaa mara kwa mara.

“Katika hoja ya uzazi, nitakapopata urais, nchi hii haitoikuwa na vitanda vya futi sita kwa sita, vitanda havitozidi futi nne, mnapokaa sita kwa sita, mama yuko kule na baba yuko kule, hamuzai. Wazee wetu zamani walikuwa wanalala kitanda futi mbili na nusu, kimezidi futi tatu, wanazaa. Leo Wazanzibari hatuzaani kwa sababu ya sita kwa sita.”

Ahadi yake imekwenda moja kwa moja kwa mafundi, akiwaambia lazima watengeneze vitanda ambavyo mwanamke na mwanaume watakaribisha uzazi wa mara kwa mara.

Mahari na Posho

sd

Chanzo cha picha, MTANDAO

Suala la ndoa limebeba umuhimu mkubwa pia. Mgombea wa urais Zanzibar, kupitia chama Makini, Ameir Hassan Ameir ameahidi mahari na posho ya miezi sita kwa kijana atakaye amua kuoa.

“Changamoto kubwa ni umasikini unaowazuia kuanzisha familia, wapo vijana wengi wanaotaka kuoa lakini hawana mahari. Chama chetu kitakapoingia madarakani, tutawapa mahari,” amesema.

Bila shaka inaonekana ni ahadi nzuri, lakini swali: Je, itakuwaje posho ikiisha baada ya miezi sita?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *